26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DC aiagiza Takukuru kuchunguza viongozi Feri

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza viongozi wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri.

Hiyo ni  baada ya baadhi ya wafanyabiashara kulalamikia kuchangishwa fedha kwa ahadi ya kupatiwa mikopo bila mafanikio.

Wafanyabiashara hao kutoka katika kanda namba tatu sokoni hapo walilalamikia kuchangishwa Sh 32,000 na viongozi wao kwa kigezo cha kupatiwa mikopo lakini hadi sasa hawajapata kitu.

Mjema alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wafanyabiashara hao sokoni hapo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo la Ilala.

“Takukuru chunguzeni kama kuna watu wamewatapeli wafanyabiashara wachukuliwe hatua za sheria.

“Ukiwa kiongozi unatakiwa uwatumikie watu lakini ukichukua fedha za wanyonge tutakutapisha,” alisema Mjema.

Pia aliuagiza uongozi wa soko hilo kumaliza kero ya wafanyabiashara kupanga samaki chini wakati kuna meza maalumu.

Mbali ya kuchangishwa fedha hizo wafanyabiashara hao pia walilalamikia utaratibu unaotumika kupata vizimba kwamba umeghubikwa na ufisadi.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Hashim Sadick alisema; Hatuna uongozi mzuri, haiwezekani ‘zone’ mama iwe maskini.

“Tuna vyama vikuu viwili lakini hatunufaiki na mikopo matokeo yake tulichangishwa fedha kila mfanyabiashara na hadi leo hakuna kinachoendelea”.

Mfanyabiashara mwingine, Juma Hamisi, aliomba waruhusiwe kuendelea kuvua Kambamti kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea aina hiyo ya uvuvi kuendesha maisha yao.

“Mimi nilianza shughuli za uvuvi tangu Julai 1974,na wakati wote nimekuwa nikivua Kambamti lakini siku hizi tumezuiwa.

“Je, tutaishije wakati tunaendesha maisha yetu kwa shughuli hizi?” alihoji Hamisi.

Akijibu kero hiyo, Ofisa Uvuvi wa Manispaa ya Ilala, Asha Zewe, alisema Serikali ilizuia uvuvi huo  kuruhusu samaki hao wazaliane.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ilifanya utafiti na kubaini viumbe hao wapo katika hatari ya kutoweka duniani.

“Hili ni agizo la Serikali baada ya utafiti uliofanywa na Tafiri uliobaini kupungua kwa Kambamti.

“Tumeuzia kuruhusu wazaliane na baada ya muda shughuli za uvuvi zitaendelea,” alisema Zewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles