25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kikao cha ndani Chadema chapigwa marufuku

Na DERICK MILTON – BARIADI


MPANGO wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kususia chaguzi za marudio na kujikita kujenga chama kuanzia ngazi ya msingi, umeingia dosari baada ya kikao cha ndani cha chama hicho kilichotarajiwa kufanyika wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu kupigwa marufuku.

Kikao hicho kilitarajiwa kufanyika Oktoba 21 na kuhudhuriwa na wanachama, viongozi wa kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga pamoja na viongozi wa Kamati Kuu.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi wa Chadema hawajatoa taarifa kwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kwenye mamlaka zinazohusika (Jeshi la Polisi) juu ya kuwepo kwa kikao hicho ili wapewe kibali.

Alisema taarifa za kiintelijensia walizopata, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na watu kati ya 500 hadi 1,000.

“Taarifa tulizonazo ni kuwa viongozi wote wa Chadema Taifa watakuwepo wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, lakini bado kama Serikali hatujapata taarifa za kuwepo kwa kikao hicho wala kuambiwa lengo lake ni nini?” alisema Kiswaga.

Alisema tayari wajumbe zaidi ya 30 wa chama hicho wameshaingia wilayani humo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kikao hicho.

“Sijapata taarifa yoyote ya kimaandishi toka kwa viongozi hao, natilia shaka kwanini wasitoe taarifa ili tutoe ulinzi, katika mkutano huo ajenda mbalimbali zitazungumzwa ambazo hazina masilahi na wananchi wa Bariadi na Simiyu ambao tuna ajenda za maendeleo.

“Tarehe hizo ambazo wamepanga kufanya mkutano huo, Wilaya na Mkoa wa Simiyu tutakuwa na maonyesho ya Sido, tutakuwa na wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa akiwemo Waziri Mkuu, kwa wingi huo Jeshi la Polisi halitaweza kutosheleza ulinzi,” alisema Kiswaga.

Alisema kutokana na hali hiyo, anapiga marufuku kikao hicho kwa sababu kina viashiria vya kuvuruga shughuli za maendeleo ya wilaya na mkoa.

Kiswaga alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD), kuhakikisha anaandaa vijana wake kwa ajili ya kufuatilia nyendo za uwepo wa kikao hicho na kuhakikisha anakamatwa mtu yeyote atakayehusika na maandalizi ya kikao hicho.

“Hata akija Mbowe atakamatwa, hata Lowassa tutamkamata, kikao chao hakina kibali na kama Serikali hatuna taarifa, hivyo kama Mkuu wa Wilaya napiga marufuku kufanyika kwa kikao hicho na kwa yeyote atakayehusika na maandalizi au kuwepo kwenye kikao hicho tutamkamata bila ya kuangalia nafasi au cheo chake,” alisema Kiswaga.

Chadema wamjibu DC

Kutokana na madai hayo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, alithibitisha kuwa wana kikao cha ndani kesho na lengo lake ni kujiandaa na chaguzi za ndani ya chama.

Mrema alisema kikao hicho cha ndani, kitafanyika huku akikanusha taarifa alizozitoa Mkuu huyo wa Wilaya kuwa kitahudhuriwa na wanachama na viongozi wa chama hicho kati ya 500 hadi 1,000.

“Ni kweli kikao kitahudhuriwa na viongozi wa Kamati Kuu Taifa wa chama wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na viongozi wengine waandamizi wa chama, lakini si kweli watu kati ya 500 hadi 1,000 watahudhuria kikao hicho, hapo Bariadi kuna ukumbi wa kumudu idadi hiyo kubwa ya watu?

“Mkuu wa Wilaya hana mamlaka ya kupiga marufuku mkutano wa ndani, mkutano huo ni haki yetu, hutuanzii Simiyu, tunafanya kanda zote, lengo ni kukipanga chama kuelekea uchaguzi wa ndani ya chama, huo ni mkutano halali.

“Mkuu huyo wa wilaya hajui sheria ya vyama vya saisa, mkutano wa ndani hauombewi kibali, anatumia sheria gani?  Akasome sheria ya vyama vya siasa, pia hakuna mahali sheria ya vyama vya siasa inapomtambua mkuu wa wilaya,” alisisitiza Mrema.

Mrema alisema Chadema kitafanya mkutano wake kama kawaida na wapo katika maandalizi ya mwisho ya kuhakikisha wanafanikisha kikao hicho huku akibainisha kuwa hawatasikiliza marufuku ya mkuu huyo wa wilaya.

Juzi Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema kwa sasa chama hicho kinaelekeza nguvu zake za kujenga chama katika maeneo yote ya nchi na kwamba tayari Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, wameshaanza ziara mikoani.

Alisema kwa sasa viongozi wengine wanakamilisha taratibu za kawaida na wote watakwenda katika mikoa tofauti kwa ajili ya mikutano ya ndani ya ujenzi wa chama hasa baada ya mikutano ya hadhara kupigwa marufuku.

“Kwa kuwa tulishatangaza kuwa hatutashiriki chaguzi za marudio, nguvu yetu sasa tunaielekeza katika kujenga chama maeneo yote ya nchi. Kwa sasa viongozi wote watakwenda kujichimbia mikoani kwa ajili ya mikutano ya ndani, kwa ajili ya kujenga chama baada ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles