TWALAD SALUM-MWANZA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, imemuhukumu mkazi wa Kijiji cha Nange, Shabo Marando (47) kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka bibi wa miaka 60.
Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi Esther Malick, ilitoa hukumu hiyo baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.
Malick akisoma hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 87 ya mwaka 2019, akichambua ushahidi wa shahidi wa tatu, Dk Judith Kiwango wa hospital ya wilaya, ambaye alimfanyia uchunguzi bibi huyo, alisema alimkuta na michubuko sehemu za siri pamoja na manii.
Shahidi wa pili ambaye ni Sama Luheka (34), mkazi wa Kitongoji cha Igokelo, Kijiji cha Nange, alisema Julai 9 mwaka huu huko Igokelo baada ya kusikia kelele katika vichaka alikwenda eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa akimbaka bibi huyo.
Naye bibi huyo aliyebakwa, kwenye ushahidi wake alidai kuwa anamfahamu mtuhumiwa kuwa ni mkazi wa kijijini kwake.
Alidai siku ya tukio alikuwa shambani akikusanya kuni na mtuhumiwa alifika na kusalimiana na mara akamkamata kwa nguvu na kumvutia kichakani na kumbaka.
Katika utetezi wake, mtuhumiwa huyo alidai kuwa mlalamikaji ni shemeji yake, alimpa eneo la kulima na siku ya tukio alikamatwa na wananchi baada ya kuwa amechota maji ya kumwagilia nyanya zake kwa madai kwamba dimbwi alilochota maji lilishazuiwa na kwamba si kweli kwamba alimbaka shemeji yake.
Awali mwendesha mashtaka wa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Juma Kiparo, akimsomea shtaka lake, alidai Julai 9 mwaka huu katika Kitongoji cha Igokelo, mtuhumiwa huku akifahamu kuwa ni kosa alimbaka bibi huyo na kumsababishia maumivu makali.