27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi awaweka mtegoni wakurugenzi wa halmashauri

Waandishi wetu-Iringa

WAZIRI wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka wakurugenzi wa halmashauri kujitathmini katika idadi ya hati za ardhi wanazotoa kwa wamiliki wa ardhi kwenye halmashauri zao.

Lukuvi alisema hayo jana katika mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kupitia programu ya Funguka kwa Waziri uliofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Manispaa ya Iringa,

Alisema wizara yake itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika upangaji, umilikishaji na utoaji hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini ambazo ziko nyuma.

 “Mkurugenzi ajione fahari kuwawezesha wananchi kwa kupima na kuwapatia hati, kama mkurugenzi huwezi kutoa hatimiliki hata mia moja basi wewe hufai,” alisema Lukuvi.

Alisema kumilikisha na kumpatia mwananchi hati ya ardhi ni kumwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati kwenye shughuli za kimaendeleo na kusisitiza kuwa wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanapanga na kuwamilikisha maeneo wananchi.

Lukuvi alisema kwa sasa wizara yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za mikoa zitakazokuwa na watendaji wote wa sekta ya ardhi kama vile wapimaji, wathamini, wataalamu wa mipango miji pamoja na wasajili.

“Sasa wapimaji, wathamini na wapangaji watakuja hapa Iringa, muundo unaanza mwezi ujao, lengo ni kuwapunguzia usumbufu wananchi katika kupata huduma za ardhi,’’ alisema Lukuvi.

Alisema katika kuboresha huduma za sekta ya ardhi, wizara yake itatumia mifumo unganishi utakaorahisisha utendaji kazi kwa wataalamu wa sekta ya ardhi ambapo kazi kubwa itakuwa ikifanyika kielektroniki badala ya kutumia makaratasi aliyoeleza kuwa wakati mwingine husababisha tamaa kwa maofisa ardhi.

Alitolea mfano Mkoa wa Dar es Salaam, umeshaanza kutumia mfumo unganishi ambapo sasa wamiliki wa ardhi wanapatiwa hati za kielektroniki na kubainisha kuwa lengo la kuwa na mfumo unganishi ni kuondoa urasimu na kurahisisha utendaji kazi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alieleza mkoa wake umejitahidi kupunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwapo miaka ya nyuma kwa kuanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao kupitia programu ya Iringa Mpya.

Alimweleza Lukuvi kama angekuja mwaka mmoja na nusu uliopita, basi ukumbi aliofanyia mkutano wa Funguka kwa Waziri ungekuwa umejaa wananchi wenye kero za ardhi, lakini jitihada za mkoa wake zimesababisha mkutano huo kutokuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye migogoro ya ardhi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Muda mwingi nautumia kwenda kwa wananchi na kazi za ardhi zina changamoto kubwa na njia pekee ya kukabiliana nazo ni kutenda haki bila kujali uwezo, kabila ama dini ya mtu,” alisema Hapi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles