25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo TFDA adaiwa kutoweka na mil. 700/-

Na ABRAHAM GWANDU-ARUSH



MHASIBU wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Kaskazini (jina linahifadhiwa), anatafutwa na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kuiba Sh milioni 703, mali ya mwajiri wake.

Taarifa za uhakika zilizolifikia MTANZANIA hivi karibuni, zinasema mhasibu huyo alitekeleza wizi huo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wenzake.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wizi huo unadaiwa kufanyika kati ya Julai, mwaka jana na Oktoba, mwaka huu.

“Yule mhasibu hakuwa peke yake katika suala hilo, bali walishirikiana na wenzake. Pia, kuna uwezekano kabisa, kwamba hata baadhi ya maofisa wa TFDA makao makuu, walishiriki maana haiwezekani wizi wa mamilioni ya kiasi hicho ufanyike bila watumishi wengine wa makao makuu kuhusika.

“Siri hii ni ya muda tu, najua ukweli wote utajulikana baada ya muda si mrefu.

“Nasema hivyo kwa sababu baada ya taarifa za upotevu wa fedha hizo kuanza kujulikana na baadhi ya watuhumiwa kuhojiwa, uongozi wa mamlaka hiyo, Kanda ya Kaskazini, uliamua kuwahamisha vituo vya kazi baadhi ya watumishi ili kujaribu kuficha ufisadi huo,” alisema mtoa taarifa huyo kwa sharti la kutotaja jina lake gazetini.

Meneja wa TFDA, Kanda ya Kaskazini, Didas Kamazima, alikiri kutokea kwa upotevu wa fedha za mamlaka hiyo, lakini akakataa kutoa maelezo ya kina kuhusu wahusika na namna tukio hilo
lilivyotokea.

“Kwa sasa siwezi kueleza zaidi kwa sababu tukio hilo tumeshaliripoti katika vyombo vya dola, naomba tuwaachie wao.

“Sitaki nilisemee sana kwa sababu nikisema zaidi, naweza kuingilia upelelezi wa tukio zima,” alisema Kamazima.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi, alithibitisha kutokea kwa wizi huo, lakini akakataa kuweka wazi majina ya watuhumiwa kwa kile alichosema ataharibu uchunguzi.

Pamoja na hayo, Kamanda Ng’anzi alisema wizi huo ulitokea mwaka mmoja uliopita baada ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo, kutumia nafasi zao vibaya.

“Ni kweli tukio hilo la wizi wa fedha za TFDA limeripotiwa hapa kwetu na Meneja wa Kanda, anaitwa Didas Kamazima.

“Kazi yetu ni kupeleleza na kuwakamata wote waliohusika na kuwafikisha mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.

“Baadhi ya watuhumiwa tumewakamata, lakini mhasibu ambaye ni mtuhumiwa namba moja, ametoweka na hajulikani alipo ila tunaendelea kumsaka ili tumuunganishe na wenzake,” alisema Kamanda Ng’anzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles