27.8 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Vigogo CUF kizimbani kwa kutishia kuua

*Yupo Mbunge ‘Bwege’,  Mkurugenzi wa Maalim Seif

*Wadaiwa kufanya uchochezi kwenye mkutano, kukashifu wana CCM

NA HADIJA OMARY-LINDI

VIONGOZI watatu wa Chama cha Wananchi (CUF), akiwamo Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara ‘Bwege’, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi na kusomewa mashtaka matatu ikiwamo la kutishia kuua.

Mbali na ‘Bwege’ wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uhusiano na Uenezi, Mbarala Maharagande pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa, Abuu Mjaka.

Washtakiwa hao walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Liliani Lugalabamo na kusomewa  mashtaka matano ambapo katika shtaka la kwanza wote wanashtakiwa kwa uchochezi.

Akiwasomea mashtaka viongozi hao Mwanasheria wa Serikali, Abdurahamani Mohamedi, alidai washtakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa Novemba 20,  mwaka huu, eneo la Kilwa  Kivinje Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Alidai washtakiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kutoa lugha ya uchochezi, kutishia kuuwa pamoja na kutoa lugha za matusi.

Mwanasheria huyo wa Serikali alidai washitakiwa wote kwa pamoja wamefanya makosa chini ya kifungu cha 390 na 89 (2) (a) Kanuni ya Uchaguzi ya 16/2015.

Hata hivyo washitakiwa wote kwa pamoja wamekana makosa waliyoshitakiwa nayo.

Mwanasheria huyo alidai mahakamani hapo kuwa katika shtaka la kwanza ni la uchochezi ambalo wameshtakiwa nalo watuhumiwa wote watatu.

“Shtaka la pili ni kutishia kuua ambalo ameshtakiwa nalo Selemani Bungara,” alisema huku akiruka shtaka la tatu kutoka na mmoja wa washtakiwa ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga, Hamid Bobali kutokuwamo mahakamani hapo.

“Shtaka la nne linamuhusu Mbarala Maharagande ambaye ameshtakiwa kwa kutishia kuua huku shtaka la tano linamuhusu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa Abuu Mjaka ambaye alitoa maneno ya matusi kwa wanachama wa CCM kwenye mkutano wa kampeni,” ilidaiwa mahakamani hapo.

Aidha katika kesi nyingine namba 11/2018, inayomkabili mbunge huyo, mwanasheria mwingine wa Serikali, Juma Maige, alimsomea mshtakiwa  kosa linalomkabili kuwa ni pamoja na kukaidi amri halali anayodaiwa kupewa na askari polisi ya kumtaka akae umbali wa mita 200 wakati wa uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya ubunge Jimbo la Liwale, uliofanyika Oktoba 13 mwaka huu.

Maige alidai kutokana na kukaidi huko, mshitakiwa alifanya makosa kwa mujibu wa kifungu cha cha 390 na 89 (2) (a) kanuni ya uchaguzi ya mwaka /2015.

Hata hivyo mshtakiwa amekana kosa na wamechukuliwa dhamana ya watu wawili kila mshitakiwa kwa dhamana ya Sh milioni moja kila mmoja. Kesi hizo namba 10 na 11/2018, ziliahirishwa hadi Desemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, wakili Rainery Songea, alisema anachoshukuru ni kwa wateja wake kupatiwa dhamana na mahakama hiyo, kwani ni haki kwa mshitakiwa, licha ya wanasheria wa Serikali kujaribu kuzuia wasipewe dhamana.

Wakili Songea alisema wateja wake wamepata dhamana, ingawa bado wapo mahabusu, kwani barua za wadhamini wao zimebainika kuwa na makosa.

Amesema wateja wake walikamatwa Novemba 21, 2018 wakidaiwa kutenda makosa mbalimbali ambayo ni kutishia, kutoa lugha isiyofaa na kushawishi watu kufanya makosa.

Songea alisema kulingana na makosa hayo, Bwege alitimiza masharti ya dhamana hiyo lakini kwa makosa mengine ambayo ametenda na wenzake alikwama.

Ametaja masharti ya dhamana ambayo washtakiwa hao walitakiwa kuyatimiza kuwa ni wadhamini wawili wanaoaminika  watakaosaini bondi ya Sh milioni moja kila moja.

Awali akizungumzia tukio hilo Mkurugenzi wa Habari, Uhusiano na Uenezi wa CUF Maalim, Salim Bimani alisema viongozi hao walikamatwa juzi kwenye viwanja vya Kivinje ambapo walikuwa kwenye uzinduzi wa kampeni za udiwani wa kata hiyo.

Alisema baada ya kuhutubia, walichukuliwa na polisi na kupelekwa kituoni ambapo wanaendelea kushikiliwa hadi kufikia jana jioni

“Ni kweli wamekamatwa juzi, walikuwa kwenye uzinduzi wa kampeni wa Udiwani wa Kata ya Kivinje na mpaka sasa bado wapo mahabusu,” alisema Bimani.

Alisema mpaka sasa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanashughulikia suala hilo ili kuhakikisha viongozi hao wanapewa dhamana au wanapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria kuliko kuwaweka muda mrefu mahabusu.

Alidai kilichofanyika ni mwendelezo wa kuvisumbua vyama vya upinzani ili visiweze kufanya kazi zao, jambo ambalo limewafanya polisi kuwakamata viongozi hao bila sababu za msingi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles