22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO ESCROW HATARINI KUPOTEZA MAISHA- WAKILI

NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

WAKILI Joseph Makandege, anayemtetea Mmiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, amesema mteja wake anaweza kupoteza maisha akiwa gerezani.

Sethi ni mtuhumiwa wa kwanza katika kashfa ya Tegeta Escrow akiwa na mwenzake James Rugemalira, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, wakikabiliwa na mashitaka 12 kwenye kesi hiyo.

Jana Makandege aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kwamba upande wa Jamhuri umeshindwa kumpeleka mteja wake kupata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na maputo aliyowekewa tumboni baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Mara mbili mahakama ilitoa amri ikielekeza utawala wa Magereza kumpeleka mshtakiwa wa kwanza (Sethi) Muhimbili , amri ilitolewa baada ya mahakama kukubaliana na hoja za upande wa utetezi, lakini badala ya kumpeleka Muhimbili, Magereza walimpeleka mshtakiwa Hospitali ya Amana.

“Ingawa mahakama yako tukufu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, inayo mamlaka ya kufuatilia mwenendo wa kesi na kuhakikisha haki inatendeka katika shauri hili, mshtakiwa wa kwanza kafanyiwa upasuaji uliosababisha kuwekewa maputo katika tumbo lake.

“Kwa taarifa za kitabibu ni kwamba hali ya mshtakiwa wa kwanza isipohudumiwa ipasavyo, inaweza kusababisha kifo kwani maputo yanaweza kupasuka tumboni.

“Mahakama ilielekeza mshtakiwa apelekwe moja kwa moja Hospitali ya Muhimbili ambayo ni hospitali ya juu kabisa ya Serikali, ndiyo nategemea inaweza kuwa na wataalamu na vifaa thabiti kwa ajili ya matatizo yanayomkabili mshtakiwa wa kwanza,” alidai Makandege.

Aliiomba mahakama itafakari kitendo cha Magereza na Jamhuri kumpeleka mshtakiwa huyo kutibiwa Hospitali ya Amana ni kwenda kinyume na amri ya mahakama.

“Walimpeleka Amana kwa kufuata amri ya nani?” alihoji.

Makandege alidai amri zote zilizotolewa na mahakama hazijatekelezwa, hivyo aliomba mahakama itoe amri nyingine ya kuutaka upande wa Jamhuri kuamuru amri iliyotolewa itekelezwe.

“Leo naomba itolewe amri hiyo, sitaki kuomba Mkuu wa Gereza kuitwa mahakamani kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua kwa kukaidi amri halali ya mahakama, nchi yetu ni ya demokrasia, inafuata utawala wa sheria, inaongozwa na kutawaliwa na utawala wa sheria, utawala wa sheria ni pamoja na kufuata na kutekeleza amri ya mahakama.

“Tunakuja mahakamani kupata haki na amri ya mahakama ndiyo ya kuheshimika, kukaidi amri ya mahakama ni dharau ya kuonyesha mahakama yako tukufu haina meno, imeng’olewa meno, kukaidi amri ya mahakama ni kosa kwa mujibu wa kifungu namba 124 cha sheria ya kanuni ya adhabu,” alisema.

Akijibu, Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter, alidai Jamhuri haijakaidi amri ya mahakama, na kwamba Magereza wana utaratibu wao wa kuhojiana na mgonjwa na wakiona tatizo lake hawana utaalamu nalo, wanampa rufaa kwenda Muhimbili.

“Magereza hawachaguliwi mahali kwa kupeleka mgonjwa, mtaalamu wao ndiye anaamua kwa kumpeleka mgonjwa ili apate huduma,” alidai Vitalis.

Wakili huyo alidai mshtakiwa huyo alipelekwa Hospitali ya Amana, ambako walipata mtaalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye alimuona na kujiridhisha kuhusu afya yake.

Baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja hizo, Wakili Makandege alidai kwamba amri ya mahakama ni mgonjwa kupelekwa Muhimbili na si kuitwa mtaalamu kwenda kumwona mgonjwa Magereza.

Akitoa uamuzi, Hakimu Shaidi, alisema ni kweli aliamuru mara mbili mshtakiwa apelekwe Muhimbili kwa matibabu na akasisitiza tena apelekwe katika hospitali hiyo ya taifa, kwani haoni shida iliyopo katika kutekeleza amri hiyo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 14, mwaka huu itakapotajwa tena.

Katika kesi hiyo Sethi na Rugemarila, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwa na mashitaka 12 yakiwemo ya kutakatisha fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles