24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kifuru kupata shule mpya ya msingi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mtaa wa Kifuru uliopo Kata ya Kinyerezi,jijini Dar es Salaam unatarajia kupata shule mpya ya msingi kutokana na inayotumika sasa kuelemewa.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mgitu, amesema tayari eneo limepatikana na wanafanya jitihada ujenzi uanze mapema ili mwakani ichukue wanafunzi.

“Tayari tumelipa fidia eneo tumemuomba mkurugenzi atupe madarasa ya kuanzia angalau matano ili mwakani shule ianze. Tuna mikakati na mipango mizuri ya kutatua changamoto zilizopo naamini mpaka 2025 tutakuwa tumepiga hatua kubwa,” amesema Leah.

Amesema mipango mingine waliyonayo ni ujenzi wa ofisi za mitaa ya Kinyerezi na kwa Limbanga, zahanati mtaa wa Kifuru na ukamilishaji ujenzi wa ofisi za serikali ya mitaa Kifuru, Kibaga, Kanga na Vichangani pamoja na uchimbaji wa visima virefu mtaa wa Kifuru na Kwa Limbanga.

Vilevile kuna ukamilishwaji wa vyoo vya soko la Kinyerezi, ujenzi wa bwawa la kufuga samaki Kanga na mradi wa mkundombinu ya maji taka unaodhaminiwa na Dawasa Mtaa wa Kanga.

Diwani huyo pia ameomba kata hiyo ipewe kipaumbele katika fedha za mfuko wa jimbo kwa sababu wana changamoto nyingi hasa za miundombinu ya barabara.

Naye Mwenyekiti wa CCM mtaa wa Kifuru, Deodatus Mvambe, ameshauri kuangaliwa upya kwa gharama za kuunganisha maji kwani zinalalamikiwa na wananchi wengi.

“Ingawa maji yanatoka lakini gharama za kuyaleta zinalalamikiwa watu hawajui zimepangwa kwa utaratibu upi ikiwezekana zipunguzwe, kama kwangu naambiwa haitapungua laki tano,” amesema Mvambe.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kinyerezi, Sam Swila, amesema visima vingi havifanyi kazi kutokana na miundombinu yake kuharibika mara kwa mara kwa kukosa watu wa kuviangalia.

Aidha amesema wameunda kamati kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na kwamba ujenzi wa ofisi ya Mtaa wa Kinyerezi tayari umepitishwa kwenye kamati ya maendeleo ya kata na eneo limepatikana.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Kinyerezi, Ambakisye Mwakisisile, amewaagiza wenyeviti wa matawi na makatibu wenezi kusimamia mitaa ipasavyo na kuhakikisha inawasilisha taarifa za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles