26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Kipunguni kuanzisha mfuko kupambana na ukatili

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni kinachojishughulisha na harakati za mapambano ya ukatili wa kijinsia kinatarajia kuanzisha mfuko kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Jamii Kipunguni unaotekelezwa na Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, Mkurugenzi wa kikundi hicho Selemani Bishangazi, amesema lengo ni kuinusuru jamii kwa kuchukua hatua za haraka pindi inapotokea mtu amefanyiwa kitendo cha ukatili.

“Tunataka kuzindua mfuko wa ukatili ikitokea shida hata kama ni kwenda hospitali tutoe huduma ya kwanza maana wakati mwingine mtu anaweza kupigwa na kuumizwa anakuja hata usafiri wa kumpeleka hospitali inakuwa ni changamoto,” amesema Bishangazi.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, amekipongeza kituo hicho kwa kupiga hatua katika kuleta mabadiliko na kuvitaka vituo vingine viige mfano huo.

“Nimefarijika sana kuona maendeleo mliyoyafikia mafanikio yako juu kuliko changamoto, naiona Kipunguni ikipiga hatua kwa njia tofauti, inataka kufanya kitu kwa ajili ya jamii pana…natamani sana vituo vingine viige,” amesema Liundi.

Aidha amempongeza Bishangazi kwa kujitoa hatua ambayo imesababisha pia wageni mbalimbali wanaokuja nchini kupenda kutembelea kituo hicho kwa kuwa kuna vitu vinaonekana.

“Bishangazi amekuwa akijitoa kwa hali na mali kwa ajili ya jamii yake Kipunguni, nafarijika sana kwa sababu ametoka mbali, uongozi si rahisi inahitaji kujitoa,” amesema.

Mlezi wa kituo hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba, ameishuri jamii kuacha kulalamika na badala yake ijitoe kwa kuhamasisha maendeleo kisha serikali ije iendeleze.

Malagashimba pia ameahidi kudhamini gharama za uanzishwaji wa tovuti ya Sauti ya Jamii Kipunguni ili shughuli zinazofanywa ziweze kuwafikia watu wengi waweze kujifunza.

Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Fatma Talib, amesema ili kupunguza utegemezi kupitia akiba walizokuwa wakijiwekea wamefanikiwa kununua jenereta, redio, hema na viti ambavyo watavitumia katika shughuli zao na kukodisha ili kujiingizia kipato.

Nao baadhi ya viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wameahidi kutumia elimu waliyoipata kutoka katika kituo hicho ili kwenda kuanzisha miradi katika maeneo yao.

Sauti ya Jamii Kipunguni ilianza kama harakati za kupinga ukatili wa kijinsia wakianza na ukeketaji lakini sasa wamejitanua ambapo pia wanatoa mafunzo ya kilimo na ushonaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles