MWANDISHI WETU
GEORGE Floyd, raia mweusi wa Marekani, kifo chake kimesababisha maandamano makubwa nchini humo. Kwa mujibu wa uchunguzi binafsi wa maiti yake, alifariki baada ya kukosa hewa safi ya oksijeni.
Floyd alifariki baada ya kukandamizwa kwa goti shingoni na mgongoni na maafisa wa polisi wa Minneapolis, uchunguzi wa kimatibabu uliosimamiwa na familia ya yake ndio ulibaini hilo.
Matokeo hayo yanatofautiana na matokeo ya uchunguzi wa mwili wake uliofanywa na madktari.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, hakukupatikana ushahidi wowote unaohusisha ukosefu wa hewa wala kunyongwa.
Matokeo ya uchunguzi huo wa kimatibabu pia yalibaini kwamba matatizo ya afya yalichangia kwa kiasi kikubwa kifo chake.
Lakini madaktari waliosimamiwa na familia ya Floyd walibaini kwamba kifo chake kilikuwa ni mauaji.
“Sababu ya kifo kwa maoni yangu kimesababishwa na ukosefu wa hewa, kutokana na kukandamizwa shingoni ambako kunaweza kutatiza oksijeni inayokwenda kwenye ubongo na kusababisha mkandamizo mgongoni, ambako kuna tatiza upumuaji,” anasema Dk. Michael Baden, aliyekuwa daktari wa Mji wa New York.
Video inayoonesha ofisa wa polisi wa kizungu akiendelea kupiga goti juu ya shingo ya George Floyd hata baada ya kusema kwamba anashindwa kupumua imesababisha hasira na ghadhabu miongoni mwa raia tangu ilipoonekana wiki moja iliyopita.
Tukio hilo limesababisha maandamano ya siku sita mfululizo nchini Marekani na machafuko ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Benjamin Crump, wakili wa familia ya Floyd, juzi alisema katika mkutano na wanahabari: ‘’Bila shaka leo hii leo angekuwa hai ikiwa hangekumbana na shinikizo la namna ile kwenye shingo yake kulikosababishwa na Derek Chauvin, aliyekuwa afisa wa polisi pamoja na mvutano uliotokea kutoka kwa maafisa wengine wawili.”
Anaongeza: “ Ambulensi ilikuwa gari ya kubeba maiti yake.”
Dkt. Baden anasema hakuwa na tatizo jingine lolote la afya ambalo huenda lingesababisha au kuchangia kutokea kwa kifo chake”.
Matokeo ya uchunguzi huo yana
hitilafiana na yale ya uchunguzi wa awali yaliyojumuishwa kwenye malalamishi ya uhalifu dhidi ya Chauvin, aliyeshtakiwa kwa mauaji ya kiwango cha tatu na kuua bila kukusudia.
Utafiti wa matibabu katika ripoti hiyo unasema kwamba Floyd alikuwa na matatizo ya moyo na kusema kuwa yote hayo yakijumuishwa pamoja, yalikuwa na uwezo wa kutatiza mfumo wake na shinikizo kutoka kwa maafisa huenda kulisababisha kifo chake.”
Matokeo kamili ya uchunguzi wa kifo chake bado hayajatolewa na ofisi ya matibabu ya kaunti ya Hennepin. Inasema kuwa inasubiri matokeo zaidi kutoka katika maabara.
Falimia ya Floyd na wakili wao inasema mashtaka dhida ya Chauvin yanastahili kuongezwa hadi kiwango cha kwanza cha mauaji.
Wanasema uchunguzi binafsi wa maiti yake unathibitisha kwamba maafisa wengine wawili waliochukua video wakati raia huyo mweusi anakandamizwa shingoni kwa goti pia nao walichangia kifo chake.
MAANDAMANO
Zaidi ya miji 75 imekumbwa na maandamano kwa sababu ya kifo cha George Floyd, mitaa ikiwa imefurika watu wanaoandamana bega kwa bega siku chache tu baada ya mitaa hiyo kuwa bila hata mmoja kwa sababu ya kuwapo kwa virusi vya corona.
Tukio la kuuawa kwa Floyd limesababisha hasira kwa jinsi maafisa wa polisi wanavyotekeza mauaji dhidi ya raia weusi ni na vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni vya ubaguzi wa rangi.
Mauaji hayo yanafuatia yale ya Michael Brown huko Ferguson, Eric Garner, New York na wengine ambayo yamesababisha kuanzishwa kwa vuguvugu la ‘Maisha ya mtu mweusi pia ni muhimu.’
Jumapili, yale ambayo yalikuwa ni maandamano ya amani yaligeuka na kuwa ghasia katika miji mingi, huku vurugu zikizuka kati ya maafisa wa polisi na waandamanaji.
Magari ya maafisa wa polisi na majengo yalichomwa moto na maduka kuporwa kwenye maeneo kadhaa. Miji mingi imeweka hatua ya kutoka nje lakini agizo hilo linakiukwa.
Jumatatu, Rais Trump aliwaambia magavana wa majimbo kwamba wamelegeza kamba na wakati unawadia wa kuchukua hatua stahiki na kutumia vizuri vikosi kutoka Jeshi la Taifa, ambapo maelfu yao tayari wamepelekwa katika majimbo mawili.
“Mnatakiwa kukamata watu, kutafuta watu na kuwafunga gerezani kwa miaka 10 na hamtawahi kushuhudia tena kitu kama hiki,” alisema Trump wakati alipofanya mkutano kwa njia ya video, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.
Kumekuwa na matukio ya ghasia katika Mji wa Washington DC, nyakati za usiku hivi karibuni, pamoja na eneo lililo karibu na Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, Trump aliahidi kutuma vikosi kumaliza maandamano hayo.
Tishio hilo lilitolewa baada ya maandamano kuzidi kuongezeka nchini humo.
Trump alisema ikiwa miji na majimbo yatashindwa kutuliza hali na kudhibiti waandamanaji kwa kutetea wakazi wake, atapeleka jeshi na kuwatatulia tatizo hilo haraka.
Alichokisema Trump
Katika Ikulu ya Marekani kwenye Bustani ya Rose, Jumatatu jioni, Trump alisema:
“Raia wote wa Marekani wameshtushwa na kifo cha George Floyd, lakini kumbukumbu hiyo haistahili kuondolewa na raia wenye ghadhabu.”
Rais Trump alielezea matukio ya uporaji na ghasia katika Mji Mkuu, Jumapili, kama aibu na kutaka usalama kuimarishwa.
“Napeleka maelfu na maelfu ya wanajeshi wenye silaha, maafisa wa jeshi na maafisa wa utekelezaji sheria kusitisha uporaji, ghasia, mashambulizi na uharibifu wa mali unaoendelea,” alisema.
Baada ya hapo akarudia angalizo kwa maandamano yanayoendelea nchini humo, na kunyooshea kidole cha lawama wanaotaka kuiangusha serikali.
Trump aliongeza kwamba: ‘’Ikiwa mji au jimbo litakataa kuchukua hatua stahiki… nitapeleka jeshi na kutatua tatizo hilo tena kwa haraka.’’
Anaongeza: “Nataka wanaopanga ugaidi huu watambue kwamba mtakabiliana na makosa kadhaa ya uhalifu.
Matamshi yake yalikosolewa na mwanachama mwandamizi wa Democrats, Joe Biden, ambaye huenda akapeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais, na kusema kuwa Trump anatumia jeshi la Marekani dhidi ya raia wa Marekani.
Kiongozi wa walio wachache katika Bunge la Seneti Chuck Schumer anasema: “Rais huyu anaweza kujidunisha kiasi gani? Matendo yake yanaonesha uhalisia wake.”
KILICHOTOKEA DAKIKA 30 ZA MWISHO KABLA YA KIFO CHAKE
Matukio yaliyosababisha kifo chake yalitokeo katika kipindi cha dakika 30.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kanda ya video na taarifa rasmi, hiki ndicho tunachokijua.
Ilianza na ripoti kuhusu noti bandia ya Dola 20. Ripoti ilitolewa jioni ya Mei 25, wakati ambapo Floyd alinunua pakiti ya sigara katika duka la Cup Foods.
Baada ya kuamini kwamba noti ya dola 20 aliyoitoa Floyd ilikuwa bandia, mfanyakazi mmoja wa duka hilo aliripoti kwa polisi.
Floyd alikuwa akiishi katika Mji wa Minneapolis, kwa miaka kadhaa baada ya kuhama kutoka Houston katika Jimbo la Texas.
Alikuwa akifanya kazi ya ulinzi mjini humo, kama mamilioni ya raia wengine wa Marekani, alikuwa amepoteza kazi yake kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Floyd alikuwa mteja katika duka la Cup Foods. ‘’Alikuwa rafiki wa duka hilo, mteja mzuri ambaye hakusababisha tatizo lolote,’’ mmiliki wa duka hilo, Mike Abumayyaleh, alikiambia chombo cha habari cha NBC.
Lakini, Abumayyaleh hakuwapo kazini siku ya tukio, wakati wa kuripoti kuhusu noti hiyo bandia, mfanyakazi wake kijana alikuwa anafuata itifaki za kazi.
Baada ya kupiga simu ya 911 mwendo 20.01, mfanyakazi huyo alimtaka Floyd kurudisha sigara hizo, lakini Floyd alikataa kurudisha kulingana na maandishi yaliotolewa na mamlaka.
Mfanyakazi huyo alisema Floyd alionekana kana kwamba amekunywa pombe na hakuweza kujizuia, yalisema maandishi hayo. Muda mfupi baada ya simu mwendo wa 20.08, maafisa wawili wa polisi waliwasili.
Floyd alikuwa ameketi na watu wengine wawili katika gari lililokuwa limeegeshwa katika kona moja.
Baada ya kulikaribia gari hilo, afisa mmoja wa polisi, Thomas Lane, alitoa bunduki yake na kumuagiza Floyd kuonyesha mikono yake.
Wakizungumza kuhusu tukio hilo, waendesha mashtaka hawakuelezea kwa nini Lane aliamua kutoa bunduki yake.
Lane, waendesha mashtaka wanasema walishika mikono ya Floyd na kumvuta nje ya gari hilo. Baadaye akakataa kufungwa pingu.
Baada ya kufungwa pingu, alikubali kushikwa huku Lane akielezea alikuwa anakamatwa kwa kutoa fedha bandia.
Ni wakati maafisa wa polisi walipojaribu kumuingiza Floyd katika gari lao ndipo mvutano ukatokea.
Mwendo wa 20.14, Floyd alikataa na kuanguka chini na kuwaambia maafisa wa polisi kwamba ana tatizo la ‘uoga ama hofu’, hii ni kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Chauvin aliwasili katika eneo hilo. Yeye na maafisa wengine walihusika katika jaribio jingine kumuingiza ndani ya gari.
Wakati wa jaribio hilo, 20.19, Chauvin alimvuta Floyd nje kutoka katika kiti cha abiria na kumuangusha chini, ripoti hiyo inasema.
Alilala hapo uso wake ukiwa chini huku bado akiwa amefungwa pingu.
Ni wakati huo ambapo mashahidi walianza kumrekodi Floyd, ambaye alionekana kuwa katika hali mbaya.
Tukio hilo lililorekodiwa katika simu nyingi na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, lilikua la mwisho kwake.
Alizuiliwa na maafisa, huku Chauvin akimwekea goti lake katikati ya kichwa chake na shingo.
‘Siwezi kupumua’, Floyd alisema na kurudia mara kwa mara, akimlilia mama yake na kusema “tafadhali, tafadhali, tafadhali…”
Kwa dakika nane na sekunde 46, Chauvin aliweka goti lake katika shingo ya Floyd, ilisema ripoti ya mwendesha mashtaka.
Dakika sita baada ya tukio hilo, tayari Floyd alikuwa amepoteza fahamu.
Katika kanda ya video ya tukio hilo, Floyd alinyamaza huku mashuhuda wakimtaka afisa huyo wa polisi kuchunguza mishipa yake ya damu iwapo bado alikuwa hai.
Mmoja wa maafisa hao, JA Kueng, alifanya hivyo, akiutazama mkono wa kulia wa Floyd, lakini hakuweza kupata mshipa hata mmoja.
Lakini, maafisa hao hawakumuachia. Mwendo wa 20.27, Chauvin aliondoa goti lake kutoka shingo ya Floyd.
Akiwa amepoteza fahamu, alipelekwa katika kituo cha afya cha Hennepin akiwa ndani ya ambyulensi.
Saa moja baadae ikatangazwa kuwa amefariki.
USIKU KABLA YA KIFO CHAKE
Inasemekana kuwa, usiku kabla ya kifo chake, alizungumza na rafiki yake mmoja wa karibu, Christopher Harris, ambaye alimshauri kuzungumza na mawakala wa kazi za muda.
‘’Kughushi, sio tabia ya Floyd. Kwa jinsi alivyofariki ni ukatili mkubwa,” alisema Harris.
FLOYD NI NANI?
Wakati wa uhai wake alikuwa anacheza soka nchini Marekani kwenye klabu ya Yates High School Lions katika Mji wa Houston mwaka 1992.
Mwaka 2007 alikamatwa kwa kosa la kupora na mahakama iliamuru kufungwa miaka mitano jela.
Hata hivyo, alikuwa anajulikana katika Mji wa Minneapolis ambapo hadi umauti unamkuta Mei 25, 2020, ni miongoni mwa watu wa Marekani ambao walikuwa wanatafuta mlo wao wa kila siku kwa kukabiliana na changamoto za maisha ya hapa na pale.
Kwa wakazi wa Houston, Texas, ambako Floyd alikulia katika miji ambayo ina idadi kubwa ya watu wenye asilia ya Afrika, Kusini mwa jiji hilo la Minneapolis wanafahamika kwa kuishi maisha ya kati.
Majina makubwa katika tasnia ya muziki nchini Marekani yameanzia huko, msanii Beyoncé amekulia katika mji huo, Drake mwanahip-hop raia wa Canada pia amekulia maeneo hayo ambayo yanaelezwa kuwa na watu wenye mawazo ya muziki wenye utamaduni wa hip-hop.
Licha ya majina makubwa kutokea huko, bado kuna changamoto kubwa kama umasikini, ubaguzi wa rangi na ukosefu wa usawa kiuchumi umekuwa siri ya wakazi katika mji huo, na miji mingine nchini Marekani.
“Muda wote nikiona mtu ambaye sio mwenyeji wa maeneo haya huwa namwambia kuwa hakuna umasikini kama ule.
“Kuna shida kubwa, ni mji wa kihuni hasa,” anasema Ronnie Lillard ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa George Floyd, wakati anazungumza na BBC.
“Bado watu wanaishi kwa shida, milio ya bunduki kawaida kabisa huku. Kuishi huku ni vigumu kukwepa matukio kama hayo,” aliongeza Lillard ambaye anaimba mziki aina ya hip-hop, akitumia jina la Reconcile.
Floyd alikuwa anajulikana katika shughuli za uratibu wa majengo, pia alikuwa kama mwandaaji wa tofali za kujengea majengo hayo na wenzake kama akina Coney Homes.
Alikuwa ni mtu mwenye miraba minne, akiwa na futi sita na nchi sita, rafiki zake waliokuwa naye utotoni wanamwelezea kama mwanamume mkamilifu zaidi kwa namna alivyojengeka akimudu vyema soka la Marekani na mpira wa kikapu.
“Tulikuwa na miaka 12 pekee, lakini yeye alionekana mkubwa kwetu, alikuwa na mguu wenye urefu wa futi sita, rafiki yake mmoja wa utotoni alimwelezea Floyd anayefahamika kwa jina la Jonathan Veal huku akisisitiza kuwa hakuwahi kumuona mtu mrefu kama yeye.
Katika timu ya John Yates High School, alikuwa akivalia jezi nambari 88, kipindi hicho anasakata kabumbu ya America, lakini baadae alionekana angefaa kucheza mpira wa kikapu katika timu ya chuo ya Florida ya Kusini ambako kwa mjibu wa CNN, alikuja kuhamia huko mwaka 1993 hadi 1995.
Alirudi tena Texas kwenye Chuo cha A&M Kingsville hata hivyo, hakumalizia masomo yake ngazi ya chuo.
Maisha ya Floyd yalibadilika ghafla mwaka 2007 baada ya kukamatwa kwa wizi na madai ya matumizi ya dawa za kulevya ambapo baadae alitupwa jela miaka mitano.
Baada ya kutumikia kifungo, alitoka na kuanza kijihusisha na shughuli za serikali ya mitaa na uokaji katika Mji wa Houston, akawa karibu na watu akijitahidi kuondoa dhana potofu dhidi yake.
Mwaka 2017 kuna video ilitoka na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii iliyokuwa inamuonyesha akiwa ameshikiria silaha, jambo lililochangia kuongeza hamu ya watoto kurudi mapema nyumbani.
Familia yake mwaka 2018 iliamia katika Mji wa Minnesota, baada ya kushawishiwa na marafiki zake na ndugu wa kiroho kupitia mpango wa kidini.
Christopher Harris, rafiki yake alisema (Floyd) alikuwa anatafuta mwanzo mpya wa maisha mapya na safari salama lakini imekatikia njiani. Alikuwa na furaha na mabadiliko aliyokuwa anayafanya.”
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa BBC.