FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
WAKATI Shule zikifunguliwa leo baada ya kupisha janga la Virusi vya corona, watainiwa wa Kidato cha Sita pamoja Vyuo vya Ualimu wanatarajia kuanza mitihani leo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, amesema kuwa mitihani hiyo itafanyika kuanzia leo Juni 29 hadi Julai 16 mwaka huu ukihusisha Shule 763, Vituo vya Watainiwa wa kujitegemea 239 na vyuo vya ualimu 85 nchi nzima.
Amesema jumla ya watainiwa 85,546 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita huku wale wa ualimu wakiwa 8,985.
“Jumla ya Watainiwa 85,546 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa kidato cha Sita mwaka huu na kati yao 74,805 ni wa shule na 10,741 ni wa kujitegemea.
“Kati ya watainiwa wa shule 74,085 waliosajiliwa, wanaume ni 42,284 swa na asiliamia 56.53 na wanawake ni 32,521 sawa na asiliami 43.47. Watainiwa wenye mahitaji maalum wapo 113 kati yao 72 ni wenye uoni hafifu, 19 ni wenye ulemavu wa kusikia na watatu ni wenye ulemavu wa akili.
“Kati ya watainiwa wa kujitegemea 10, 741 waliosajiliwa, wanaume ni 7,109 sawa na asilimia 66.19 na wanawake ni 3,632 sawa na asilimia 33.81, aidha watainiwa wa kujitegemea wenyewe uoni hafifu ni wawili na wasiona ni mmoja,” alisema Dk. Msonde.
Kuhusu Mtihani wa Ualimu amesema Jumla ya watainiwa 8,985 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kozi za ualimu ambapo kati yao 3,268 ni ngazi ya Stashahada na 5,717 ni ngazi ya Cheti.
“Kati ya watainiwa 3,268 wa ngazi ya Stashahada waliosajiliwa , 1m996 sawa na asilia 61.08 ni wanaume na 1,272 sawa na asiliami 38.92 ni wanawake, aidha kati ya watainiwa 5,717 wa ngazi ya Cheti waliosajiliwa, 2,729 sawa na asiliami 47.73 ni wanaume na 2,988 sawa na asiliami 52.27 ni wanawake,” alisema Dk. Msonde.
Akizungumzia maandalizi kuelekea kwenye mitihani hiyo, Dk. Msonde amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambaza kwa mitihnai husika, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani hiyo nchi nzima.
“Mitihani hii ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kuwa hupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi katika yale yote waliyojitunza kwa kipindi cha miaka miwili ya elimu ya Sekondari ya juu. aidha, matokeo ye mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati katika fani mbalimbali za utaalam wa kazi kama vile Afya, Kilimo, Ualimu, Ufundi na nyingine.
“Hivyo mtihani huu ni muhimu sana kwa wanafunzi, wazazi, jamii nzima na Taifa kwa ujumla, aidha matokeo ya mtihani wa ualimu husaidia kupatikana kwa walimu ambao hufundisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari,” amesema Dk. Msonde.
Aidha, ametoa wito kwa amati za mitihani za mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya taifa zinazingatiwa.
“Kamati zihakikishe kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu.
“Kamati zote pia zinaelekezwa pia kuhakikisha usalama wa vituo teule unaimarishwa na kwamba vituo vitumike kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Baraza la mitihani la taifa.
“Baraza linawaasa wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule, walimu na wananchi wote kwa uumla kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mitihani, hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha au kusababisha udanganyifu wa mitihani ,” amesema Dk. Msonde.