25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waliopimiwa ardhi bila kuchukua hati kuanza kulipa kodi

Na Mwandishi Wetu- Njombe

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula amesema kuanzi Julai mosi, mwaka huu, wananchi wote wasiochukua hati za ardhi, huku maeneo yao yakiwa yamepimwa na michoro yake kuidhinishwa wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi.

Hatua hiyo, inatokana na Bunge la 11la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria inayomtaka mwananchi aliyepimiwa ardhi na michoro kuidhinishwa kuchukua hati kipindi kisichozidi 90 na asipofanya hivyo ataanza kudaiwa kodi ya ardhi.

Akizungumza na wananchi mkoani Njombe jana, wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi ya mkoa  huo, Mabula alisema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi  kukwepa kuchukua hati za ardhi wakati taratibu zote zikiwa zimekamilika, ikiwemo  kuidhinishwa michoro na kuwekewa alama za mawe.

Dk. Mabula alisema Julai mosi mwaka huu, muarobaini kwa wamiliki wasiotaka kuchukua hati za ardhi umefika kwa kuwa atakayeshindwa kuchukua hati atalazimika kudaiwa kodi kuanzia pale michoro yake ilipoidhinshwa.

‘’Kuanzia sasa wamiliki wa ardhi hapa Njombe ambao wamepimiwa na michoro yao kuidhinishwa waende halmashauri za wilaya kurekebisha kumbukumbu zao na baada ya hapo asiyerekebisha baada ya siku tisini tunaanza kumdai,” alisema.

Aliwaagiza maofisa ardhi  halmashauri za wilaya kuhakikisha kuanzia Julai mosi wanawapelekea hati ya madai wale wote waliopimiwa na michoro kuidhinishwa ili waanze kulipa kodi ya pango la ardhi.

Alisemapamoja na wananchi wakiwemo wa Njombe kufurahia usogezwaji huduma za sekta ya ardhi karibu,lazima wawajibike kwa kulipa kodi ya ardhi na kupatiwa hati aliyoieleza  inaongeza thamani ya ardhi sambamba na hati miliki yake kutumika katika shughuli za kiuchumi.

Alizitaka ofisi za ardhi katika  halmashauri zote kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo yao kuhusiana na umuhimu wa kuchukua hati ili kujua takwa la kisheria hasa ikizingatiwa wengi wao wameshindwa kuchukua hati kwa sababu mbalimbali.

Kuhusu uchukuaji hati za ardhi, alisema mkoa huo una hati 42,516 zilizoidhinishwa,kati ya hizo ni 11,246 tu ndizo wamiliki wake walijitokeza kuzichukua huku wamiliki 31,270 wakiwa hawajachukua.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Lucy Msafiri aliyemwakilisha mkuu wa mkoa, alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi katika mkoa huo,kutaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika masuala ya ardhi kwenye mkoa huo.

Alisema Njombe ni maarufu kwa kilimo cha miti,chai, mahindi, viazi na parachichi na baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo hawana hati miliki za ardhi,uanzishwaji ofisi hizo unafungua milango kwa wamiliki wa mashamba  kumilikishwa kwa haraka.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Wilson Ruge ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa ni moja ya mikakati iliyopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa tayari kazi kubwa imefanyika ikiwemo usambazaji vifaa na kuwataka wananchi kujitokeza kumilikishwa ardhi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles