30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Mama atuhumiwa mchawi, auawa

Na Gurian Adolf-Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linawasaka watu wasiojulikana kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga mawe, Maria Birika(40) mkazi wa Kijiji cha Myunga,wilayani Kalambo akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina.

Tukio la mauaji ya Maria lilitokea Juni 26, mwaka huu  saa 12:00 jioni, baada ya watu watuhumiwa kufika nyumbani kwa Maria na kukumkuta mtoto Given Lameck, akiwa amefungiwa nyumbani kwa mwanamke huyo, huku akiwa amefungwa kitambaa chekundu usoni.

Kabla ya mauaji hayo, Given alipotea nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha, ndipo harakati za kumtafuta zilipoanza ambapo ndugu zake walimtafuta muda mrefu bila mafanikio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo alisema baada ya jitihada za kumpata mtoto kugongwa mwamba, waliamua kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji kuhusu tukio la kupotea kwa mtoto,kisha kuendelea kumtafuta.

Alisema  baada ya kumtafuta muda mrefu, walifanikiwa kumkuta nyumbani kwa Maria akiwa amefungiwa ndani na amefungwa kitambaa chekundu usoni, huku akionekana amechanganyikiwa kutokana na kuzungumza vitu visivyo eleweka.

Baada ya kupatikana mtoto,ndipo watu waliokuwa wakimtafuta walihamaki na kushikwa na hasira na kuanza kumpiga Maria  kwa mawe na vipande vya matofali vilivyokuwa karibu na nyumba yake na kumsababishia majeraha makubwa,kuvuja damu nyingi na kufariki dunia kutokana na kukosa matibabu ya haraka.

Kamanda Masejo alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuachana na imani za kishirikina katika matukio yanayotokea mkoani humo,kwani imani hizo zimekuwa chanzo cha vifo vingi na sababu ya kujichukulia sheria mikononi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,873FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles