Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Winga wa JKT Tanzania, Shiza Kichuya amesema msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara anatamani kumaliza na mabao kuanzia matano kwenda juu kutokana na msimu uliopita kushindwa kufanya hivyo.
Akizungumza na Mtanzania Digital, leo Septemba 18,2024, wakati wa Media Day ya JKT Tanzania, amesema msimu uliopita ulikuwa mgumu kwake lakini kwa sasa yuko vizuri na ligi ndiyo imeanza, hivyo amejipanga kutimiza malengo yake.
“Mimi najivuniaga kuwa nikiwa fiti nikimaliza ligi bila kuwa na goli nane, tisa au kumi na ninafanya hivyo, nasemaga kabisa ligi hii lazima nimalize na goli hizo. Kwa winga kumaliza na goli kama hizo pia ni jambo kubwa kwa sababu uko mbali na goli,”
amesema Kichuya.
Ameeleza kuwa msimu uliopita alitoka Namungo na kujiunga na JKT Tanzania kipindi cha dirisha dogo alikuwa hajafunga bao lolote na akamaliza msimu patupu.
Aidha amefafanua kuwa kikosi chaa cha JKT Tanzania msimu huu kimesheni wachezaji wazuri, hali inayomfanya mwali awe na wakati mgumu wa kuchagua ni nani aanze naye katika mechi.
“Kwa upande wangu muda wowote nipo katika mapambano. Katika timu yetu hakuna mchezaji tegemeo kila mchezaji ni tegemeo, sisi wachezaji tumekaa tunashauliana ili kuendelea kumpa kazi mwalimu ya kuchagua nani aanze,”
“Sasa hivi timu yetu ina kila aina ya mchezaji ambaye mwalimu au uongozi unamtaka. Hadi sasa hivi tunaendelea vizuri kutokana na wachezaji waliopo, wazoefu na vijana,” ameeleza.