25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

KIBUBU; MBINU MPYA YA KUKUSANYA DAMU SALAMA PWANI

Na VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA PWANI


WATU wengi humiliki vibubu (visanduku) majumbani kwa ajili ya kuhifadhi fedha ili ziwasaidie pale inapotokea wamepata tatizo kubwa.

Lakini hii ni tofauti kwa wakazi wa Pwani, katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kuna kibubu kilichopakwa rangi ya bluu na kuandikwa maneno kwa rangi nyeupe yanayosema; ‘changia damu, okoa maisha’

na juu yake kumebandikwa karatasi nyeupe iliyoandikwa maneno yanayohamasisha watu kuchangia kiasi chochote alichonacho.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Shirika la Elimu Kibaha, Lucy Semindu anaelezea historia ya hospitali hiyo akisema ilianzishwa mwaka 1967 ikiwa kituo cha kutolea huduma chini ya Shirika la Elimu Kibaha.

Anasema baadae ilipandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya na kupandishwa tena hadhi kuwa Hospitali ya Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani mwaka 2011.

“Hadi sasa ipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha,  imekuwa ikipokea wagonjwa wengi hasa watokanao na ajali za barabarani katika barabara ya Morogoro.

“Kwa siku hupokelewa majeruhi kati ya 10 hadi 15; kipindi cha nyuma wengi walitokana na ajali za mabasi makubwa, wenzetu Jeshi la Polisi walifanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii na mbinu za kudhibiti ajali.

“Bado kuna changamoto, hivi sasa kwa siku tunapokea majeruhi kati ya 10 hadi 15 ambao wanatokana na ajali za pikipiki maarufu bodaboda,” anasema.

Anasema kwa kuwa huwa wanapokea majeruhi wengi, kuna uhitaji mkubwa wa damu ndiyo maana walianzisha kitengo cha damu salama hospitalini hapo.

 

Hali ya ukusanyaji damu 

Anasema kitengo hicho kila mwezi hukusanya chupa 210 hadi 270 ambazo hutosheleza mahitaji ya hospitali hiyo.

“Licha ya kwamba huwa tunapata damu kutoka kwa ndugu wa wagonjwa, damu nyingi hupatikana pale ambapo kitengo hiki hufanya ‘out reach program’ kwa kwenda shuleni, makanisani na misikikitini,” anasema.

Anasema damu inayokusanywa kutoka kwa ndugu wa wagonjwa ambao wamelazwa wodini huwa ni kati ya chupa 70 hadi 90 pekee.

Anasema damu nyingi tunayoitegemea ni ile inayokusanywa shuleni, makanisani na misikikitini kwa kuwa huwa ni salama zaidi kuliko ile inayokusanywa kwa ndugu wa wagonjwa.

“Wengi wanajitolea lakini baadae huwa haitumiki, huwa zina madhara… tunapokusanya huwa tunalazimika kupeleka sampuli benki kuu ya damu salama kwa vipimo zaidi kabla ya kuitumia.

“Unaweza kupata chupa 60 kwa ndugu wa wagonjwa lakini zikipimwa unakuta chupa 30 si nzuri, inabidi ziharibiwe,” anabainisha.

Akizungumzia suala la bajeti Semindu anasema kitengo hicho kinapaswa kupangiwa bajeti ya kutosha kwa ajili ya kukusanya damu.

“Tunanunua maji na wanafunzi huwa tunawapa vitu mbalimbali ikiwamo madaftari, kalamu na vinginevyo ili kuwahamasisha waendelee kujitolea damu.

“Kitengo hiki kimekuwa msaada mkubwa kwa hospitali ya Tumbi na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Mloganzila.

“Huduma inapatikana hapa hapa Tumbi na huwa tunawasaidia damu Hospitali ya Mlandizi, Hospitali ya Mkoa na zingine za binafsi pale wanapokuwa na uhitaji,” anasema.

 

Sababu ya kuweka kibubu

Anasema ni njia ya kuwahamasisha watu kuchangia, si hawajitoshelezi bali kupata ziada huleta moyo zaidi.

Semindu anasema: “Mwengine anapochangia hapendi jina lake litajwe, tumeanza kutumia njia hii tangu mwaka jana, inasaidia kwa kiasi fulani na bado tunahamisha watu wachangie.

 

“Hatulazimishi mtu ni kama kutoa sadaka tu, au unakuta mabango yamebandikwa kuhamasisha kuchangia damu kwa hiyo ni mtu mwenyewe aguswe kuchangia, anaweza kuchangia damu au kiasi chochote cha fedha ili kuwezesha kununua viburudisho kwa ajili ya wanaochangia,” anasema.

 

Kuitunza ni gharama 

Semindu anasema kuitunza damu iliyokusanywa ili  ifae kwa matumizi ni gharama kubwa.

“Hospitali hutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mifuko ya kuhifadhi na kuitunza, pia huwa tunapata ufadhili wa mifuko kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama na wakati mwingine hospitali hupata fedha kutoka Serikali Kuu,” anasema.

Anasisitiza japo hutumia gharama kukusanya damu huwa hawauzi, wanaohitaji wanapata huduma hiyo bure kwa mujibu wa miongozo ya serikali, mahitaji halisi kwa hospitali ya Tumbi na zingine zinazoizunguka Mkoa wa Pwani kwa mwezi ni chupa 240 hadi 300 na hatujawahi kupungukiwa.

 

Hali halisi nchini

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) inapendekezwa kila nchi iwe na hifadhi ya damu kwa kiwango cha asilimia moja ya idadi ya watu wake ili kuweza kutosheleza mahitaji.

Kwa uwiano huo, Tanzania inapaswa kukusanya chupa za damu 500,000 kila mwaka, lakini Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini haijawahi kufikia kiwango hicho cha ukusanyaji wa damu nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema takwimu za ripoti ya mwaka 2016 zinaonesha jumla ya chupa za damu 196,735 zilikusanywa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba.

“Ingawa inaonesha kuongezeka kwa makusanyo ya damu zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na chupa za damu 65,000 ambazo zilikusanywa mwaka 2015, bado kuna changamoto,” anasema.

Anasema mahitaji ya damu ni makubwa nchini hasa kwa kundi la wanawake ambao wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua.

Anasema kama kungekuwa na akiba ya kutosha ya damu, wanawake wengi wasigepoteza maisha.

Anabainisha kuwa takwimu za hivi karibuni zinaonyesha takribani wanawake 556 kati ya vizazi hai 100,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi nchini na inakadiriwa asilimia 40 ya vifo hivyo vingeweza kuepukika kama kungekuwa na akiba ya kutosha ya damu salama.

“Kwenye bajeti ya mwaka 2017/18 serikali imeongeza kiwango cha fedha kutoka Sh bilioni 4.5 hadi Sh bilioni 5.5 kwa ajili ya Mpango Taifa wa Damu Salama,” anasema.

Anasema pamoja na hatua hizo bado ni vema halmashauri zote nchini zikatenga bajeti kwa ajili ya kununulia vifaa vya kukusanyia damu.

“Kila mkoa na halmashauri inapaswa kuhakikisha hospitali zake zinakuwa na damu salama wakati wote.

 

“Viongozi wa mikoa na halmashauri waweke utaratibu wa  kukusanya damu kutoka kwa wachangia damu wa hiari na kuacha  tabia ya kutegemea kupata damu kutoka kwa wachangia damu wanandugu (Family replacement donors).

“Ndugu kuchangia damu uwe ni utaratibu wa dharura ambao wakati mwingine si salama kwani hulazimika kuchangia hata kama hawana vigezo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles