23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

KIBOSILE ‘ANAYEFUGA’ WASICHANA MITHIRI YA MBWA

Pretty-Mike-Lagos-600x600

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI,

MMILIKI wa klabu moja ya usiku mjini Lagos, Nigeria, Mike Eze-Nwalie Nwogu hivi majuzi alikamatwa na polisi kwa kosa la kuwadhalilisha wasichana wadogo.

Mmiliki huyo mwenza alikuwa akiwafunga wasichana hao kamba kuzunguka shingo yao mithiri ya mbwa na kuzunguka nao mitaani au katika kumbi hadharani.

Nwogu, ambaye anajulikama kwa jina maarufu la ‘Pretty Mike’ miongoni mwa wana mitandao ya jamii wa jiji hilo la kibiashara Nigeria, aliwageuza wasichana wadogo kama “mbwa wa kibinadamu’ kwa mwaka mmoja sasa.

Alipoonekana mara ya kwanza kama ‘bwana mbwa’ aliyeshikilia ‘mbwa’ mwaka jana, wakati akihudhuria harusi moja, picha zilizochukuliwa katika hatua hizo hazikupewa uzito mkubwa.

Hilo liliaminika kuchochea azma yake ya kuendelea tabia yake hiyo, mara kwa mara kuionesha hadharani tangu siku hiyo.

Hivyo, mwonekano wake huo wenye utata ukaanza kusababisha mijadala katika mitandao, huku watumiaji wengi mitandao ya jamii wakilalamika kuwa kitendo hicho hakina maana zaidi ya kuwadhalilisha wanawake.

Sasa picha ya Pretty Mike akiwashika wasichana wawili kwa kamba huku macho ya maofisa watano wa polisi wakifuatilia na kucheka kioja hicho ikaongeza ukali wa mjadala.

Picha zaidi zilionesha Nwogu akitembea na wanawake waliofungwa kwa ugwe au ukanda na kusababisha hasira katika mitandao ya jamii huku watu wengi wakieleza kutofurahishwa na vitendo hivyo.

Na baadhi walitaka mamlaka za jimbo kuchukua hatua dhidi ya mwanaume huyo mdhalilishi.

Ijapokuwa awali hakukuwa na mwitikio wa mamlaka za kiserikali wala polisi, kelele za umma zikawa kubwa mno kiasi cha kulazimika kumkamata.

“Kwanini wengi walikuwa kimya katika suala hili? Si waigizaji? Wanamuziki, wanamitindo wala maofisa wa kuchaguliwa?” mwigizaji wa Nollywood, Georgina Onuoha aliandika mtandaoni.

“Lini jamii yetu imefikia hatua ya kufumbia macho vitendo viovu kimaadili na haramu kiasi hiki? lini sisi kama taifa tumefikia hatua hii ya unyama? Alihoji.

“Iwapo angekuwapo mzungu leo hii katika mitaa ya Lagos anayefunga wasichana au wavulana wawili weusi mithili ya mbwa; naapa tungepinga kudhalilishwa na kutoa wito wa hatua kali za kisheria, hivyo je, tunadhani hii ni sahihi? Au kwa sababu yeye ni mtu mweusi?” aliongeza.

“Kile anachofanya Pretty Mike kinaweza kisiwe uvunjaji wa sheria, lakini kudhalilisha watu kwa kiwango hicho, yeyote mwenye akili zake timamu angekilaani vikali,” mchangiaji mwingine alisema.

“Wasichana wanahitaji kuwezeshwa. Kuna zaidi ya hili la kutendwa kama mbwa,” alisema mchangiaji mwingine Mercy Okam.

Mmiliki huyo mwenza mwenye umri wa miaka 30 wa Klabu ya UNO alikamatwa na polisi Jumatano wiki iliyopita, kwa agizo la Serikali ya Jimbo la Lagos.

“Serikali ya Jimbo la Lagos imedhamiria kulinda haki za raia wote ikiwamo watoto, wanawake na watu wote wanyonge jimboni,” ofisa mmoja wa serikali alisema.

Pretty Mike aliachiwa hata hivyo muda mfupi baada ya kukamatwa. Ni baada ya kutakiwa kusaini nyaraka akiapa kutorudia tena kitendo cha kuwafunga wanawake au wanaume kwa ugwe, au kuwatenda kwa namna ya kudhalilisha.

“Mimi, Mike Eze Nwalie, A.K.A Pretty Mike wa 21A Magodo GRA, Mtaa wa Luma, naapa kutorudia vitendo vya kuwafunga wasichana kwa ukanda au hali yoyote ya kuwadhalilisha wanawake au wanaume,” kiapo chake kilisomeka.

“Nafahamu kwamba vitendo hivyo ni ukiukaji wa sheria za Jimbo la Lagos na iwapo nitarudia tena, nitachukuliwa hatua kali za kisheria. Nachukua nafasi hii kuomba radhi kwa umma na mitandao yote ya jamii kuanzia kesho.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles