Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta vyuo vikuu viwili, kusimamisha utoaji wa masomo kwa vyuo vikuu vitano na kuzuia udahili wa wanafunzi wapya kwa vyuo saba.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema hiyo ni kutokana na upungufu mbalimbali uliobainika baada ya uchunguzi uliofanywa mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alivitaja vyuo vilivyofutwa kuwa ni Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji kituo cha Tabora (TEKU Tabora) na Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania (kituo cha Msalato – SJUT).
Alisema TCU pia imesimamisha utoaji mafunzo kwa ngazi zote katika vyuo vitano na kuamuru wanafunzi wake wahamishiwe kwenye vyuo vingine.
Vyuo hivyo ni Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB), Chuo Kikuu cha Eckernforde Tanga (ETU), Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta kituo cha Arusha (JKUAT) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JOKUCo).
Pia alisema tume imezuia udahili wa wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo na katika programu zote katika vyuo vikuu saba.
Alitaja vyuo hivyo kuwa ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian (MARUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (CARUMUCo), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastina Kolowa (SEKOMU), Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania (kituo cha Mt. Marko SJUT) na Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT).
“Asitokee mwanafunzi yeyote akasajiliwa katika vyuo hivyo na wanaotakiwa kuhama wawasiliane na vyuo vyao haraka,” alisema Prof. Kihampa.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ukaguzi uliofanyika mwaka 2016 ambao ulibaini upungufu kwenye vyuo mbalimbali na ambavyo vilipewa muda wa kufanya marekebisho.
Tume imevitaka vyuo vikuu vyote vilivyotajwa katika taarifa hiyo kuzingatia na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa.
Vilevile wanafunzi wanaotakiwa kuhama kuwasiliana na vyuo vyao kwa ajili ya maelekezo kuhusu taratibu za kuhama na vyuo wanavyotakiwa kuhamia.
Naye Mwakilishi Bodi ya Mikopo, Deus Changala alisema waliokuwa na mikopo wasiwe na wasiwasi kwa sababu itapelekwa watakapokuwa.
Julai 18, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema katika mwaka wa masomo wa 2018/2019 baadhi ya vyuo havitaruhusiwa kudahili wanafunzi.
Profesa Ndalichako alisema katika kutimiza azma hiyo, tayari Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira tawi la Mbeya na Jomo Kenyatta tawi la Arusha vimefutwa rasmi.
Alisema hakuna sababu ya kuwa na orodha ndefu ya vyuo ambavyo havina ubora na kuonya atakayefutiwa chuo asiende kumwona.
“Serikali haiwezi kuvumilia chuo kitakachoendesha mafunzo kinyume na taratibu. TCU endeleeni kukagua na kuchukua hatua.
“Hata kama ni chuo cha umma, kama hakina vigezo funga kwa sababu mimi ndiye waziri mwenye dhamana na ndiye nitakayeweza kulisemea kama nikiulizwa.
“Inakuwaje kila siku kuna wahitimu wanamaliza elimu ya juu hawawezi hata kuandika barua ya kazi halafu TCU na NACTE (Baraza la Taila na Ufundi) mpo?
“Hatuna sababu ya kuwa na orodha ya vyuo vingi ambavyo havina ubora na hata katika mwaka huu vyuo vingi havitaruhusiwa kudahili,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema mwaka juzi, vyuo 98 vinavyotoa shahada vilikaguliwa na mwaka jana vyuo 406 vinavyotoa mafunzo ya kati vilikaguliwa na vyuo 19 vilisimamishwa kudahili huku programu 75 zikizuiwa kuchukua wanafunzi kwa sababu zilianzishwa kwa kutofuata utaratibu.
Julai 2017, TCU ilitangaza kufungia vyuo 19 kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18, huku ikifungia fani 75 kutoka kwenye vyuo 22 vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kile cha Mzumbe.
“TCU inapenda kuuarifu umma kuwa Septemba na Oktoba mwaka 2016 ilifanya uhakiki wa vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa vyuoni,” ilisema taarifa ya TCU.
Kutokana na uhakiki huo, TCU ilisimamisha udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18 kwa vyuo vya Eckenforde (Tanga)
Jomo Kenyatta (Arusha) Kenyatta (Arusha) na United African University of Tanzania.
Vingine ni International Medical and Technological University (IMTU), University of Bagamoyo, St. Francis University College of Health and Allied Sciences, Archbishop James University College na Archbishop Mihayo University College.
Ilivitaja vingine kuwa ni Cardinal Rugambwa Memorial University College, Kampala International University Dsm College, Marian University College, St. Johns University of Tanzania Msalato Centre, St. Johns University of Tanzania, Marks Centre, St. Joseph University College of Engineering and Technology, Teofilo Kisanji University, Teofilo Kisanji University Tabora Centre, Tumaini University, Mbeya Centre na Kilimanjaro Christian Medical University College (KCMCo).
“Kutokana na upungufu katika vyuo mbalimbali imeamriwa kwamba programu 75 kutoka vyuo 22 nchini zimesimamishwa kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18.
“Tume inapenda kusisitiza kwamba uamuzi huu hautawahusu wanafunzi wanaondelea na masomo katika programu na vyuo husika,” ilisema taarifa hiyo.