Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KITENDO cha Mke wa Rais John Magufuli, Janeth, kulazwa wiki hii katika Wodi ya Sewahaji, iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kimejenga hisia kwamba pengine sasa itakuwa ni marufuku kwa vigogo serikalini kutibiwa holela nje ya nchi.
Hisia hizo zinatokana na si tu kitendo cha Mama Janeth kulazwa Muhimbili, bali pia mwenendo wa Serikali ya Rais Magufuli, ambao umejipambanua kuja kusafisha nchi na kubana matumizi yasiyo ya lazima.
Katika misingi kama hiyo, huenda sasa marufuku hiyo itawagusa zaidi baadhi ya vigogo ambao kutokana na hadhi zao, walizoea kwenda kutibiwa katika hospitali za nje ya nchi kwa gharama za Serikali, ilhali maradhi yanayowasumbua yanaweza kutibiwa na madaktari bingwa wanaopatikana MNH.
Wakati kukiwa na hisia kama hizo, taarifa za hivi karibuni kabisa ambazo gazeti hili limezipata lakini hazijaweza kuthibitishwa na mamlaka husika, zinaeleza kuwa, tayari kiongozi mmoja mwandamizi amenyimwa dola za Marekani 200,000, ambazo ni sawa na zaidi ya Sh 400,000,000, kwa ajili ya kwenda kutibiwa nchini Ujerumani.
Watu wa karibu na kigogo huyo walilieleza MTANZANIA Jumapili kuwa, huenda kukataliwa kwake huko kumetokana na msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kubana matumizi.
Taarifa hiyo inatiwa nguvu na kauli iliyopata kutolewa Agosti mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye aliitaka Muhimbili kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi ili kuipunguzia Serikali gharama.
Mara kadhaa Ummy amesikika akisisitiza dhamira ya Serikali katika kujenga uwezo wa ndani kwa kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuongeza idadi ya madaktari bingwa ili kuweza kusimamia kwa ukamilifu tiba hapa nchini.
Pia alisema deni la wizara litapungua kwa kuwa asilimia 90 ya safari za matibabu ya nje ya nchi anazoidhinisha kwa sasa hazilipiwi na Serikali.
Kwa mujibu wa Ummy, Serikali imekuwa ikitumia kati ya Sh bilioni 20 -25 kwa mwaka kwa ajili ya matibabu nje ya nchi.
Kwa kawaida utaratibu wa Serikali kulipia gharama za matibabu za viongozi wake nje ya nchi umelenga zaidi maradhi ambayo yameshindikana kutibiwa hapa nchini na si vinginevyo.
Katika ripoti yake aliyoiwasilisha mwaka huu, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, inaonyesha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, deni la matibabu katika hospitali mbalimbali za nchini India liliongezeka kutoka Sh bilioni 17 za mwaka wa fedha wa 2013/2014 hadi kufikia Sh bilioni 28.
Pia ripoti hiyo ilitaja baadhi ya hospitali zilizoko nchini India zinazoidai Serikali kuwa ni pamoja na Apollo Hyderabad ambayo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 deni lilikuwa Sh bilioni 2.7, lakini hadi kufikia Aprili, mwaka huu lilipaa na kufikia Sh bilioni 4.8.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Hospitali ya Apollo Chennai, ambayo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 ilikuwa inadai Sh bilioni 6.6, mwaka huu deni limeongezeka na kufikia Sh bilioni 8.7.
Hospitali nyingine inayoidai Serikali ni Apollo Bangalore, ambayo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 deni lilikuwa Sh milioni 380 na mwaka wa fedha wa 2014/2015 likapanda na kufikia Sh bilioni 1.2.
Pia Hospitali ya Apollo Ahmedabad ilikuwa inaidai Serikali deni la Sh milioni 582, lakini kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 lilipanda hadi Sh bilioni mbili.
Wakati hali halisi ikiwa hivyo, kitendo cha Rais Magufuli kuruhusu mkewe alazwe MNH kimetoa changamoto kubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika ambazo viongozi wake na baadhi ya vigogo serikalini hupenda kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Tayari kupitia picha ya Mama Janeth akijuliwa hali na Rais Magufuli, iliyosambaa kwa kasi na kuvuka mipaka ya nchi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, imesababisha maoni na mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi mbalimbali wa Afrika Mashariki, hususan nchini Kenya.
Moja ya mitandao iliyoweka picha hiyo ya Mama Janeth akiwa amelazwa MNH ni Blogu ya The Star, ambayo mwandishi wake anasema Magufuli ametoa changamoto kwa nchi za Afrika kuthamini vya kwao.
Katika andiko lake hilo, mwandishi huyo alieleza kuwa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta iliyoko nchini Kenya ina hadhi sawa na MNH, lakini viongozi wengi hawaitumii.
Alisema picha hiyo imeleta changamoto, ikiwa ni hivi karibuni Gavana wa Bomet, Issac Rutto, alikwenda kupata tiba ya jeraha la jicho nchini Afrika Kusini.
Pia blogu hiyo ilizidi kudai kuwa Agosti, mwaka huu, Rais mstaafu Mwai Kibaki alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa wa mshipa wa shingo katika hospitali moja iliyoko nchini Afrika Kusini.