24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mch. KKKT amchapa makofi mwanahabari

Askofu Alex Malasusa
Askofu Alex Malasusa

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

MCHUNGAJI Emmanuel Majora wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Usharika wa Usa River, wilayani Arumeru, mkoani hapa, ameweka kando hekima za Mungu na kumchapa makofi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Luninga cha Star Tv, Theodora Mrema.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana mchana kanisani hapo, wakati wa purukushani zilizohusisha pande mbili zilizokuwa zikivutana juu ya uhalali wa ndoa iliyokuwa inatakiwa kufungwa kati  ya Bwana Harusi Ngarame Meena na Bibi harusi Agnes Kaaya.

Hata hivyo, ndoa hiyo ilijikuta ikiingia balaa baada ya upande wa pili wa mwanamke aliyejulikana kwa jina la Aneth Kimaro, kudai kuwa Bwana Harusi ni mume wake wa ndoa hivyo hakuwa tayari kuona ndoa hiyo ikifungwa.

Kutokana na taarifa hizo, baadhi ya waandishi wa habari mjini hapa walilazimika kwenda kanisani hapo ili kuzungumza na viongozi wa kanisa juu ya sakata hilo la ndoa, lakini pia kuona kitakachokuwa kimejitokeza kanisani hapo.

Ilipofika majira ya mchana, waandishi wa habari wakiwa na waumini wengine, Aneth, aliyedai ni mke wa Bwana Harusi, akiwa na watu wake walianzisha vurugu iliyosababisha Bibi Harusi na Bwana Harusi kutawanyika kila mtu kivyake.

Kutokana na vurugu hizo, Theodora alikuwa akipiga picha za video kwa ajili ya chombo chake, wakati askari polisi wakiwapakiza kwenye gari wanawake waliofanya fujo.

“Nilikuwa napiga picha za wanawake kupakizwa kwenye gari la polisi, ghafla alikuja Mchungaji na kunikamata kichwani kwa nguvu kisha kanizaba vibao huku wengine wakinishambulia,” alidai Theodora na kuongeza:

“ Viongozi hao wa dini walikuwa wakinishambulia huku wakitaka kuninyang’anya kamera, huku baadhi ya watu wakiwa wamesimama nje ya geti wakipiga kelele za kuomba niachiwe,” alisema.

Aliendelea kudai kuwa, wakati tukio hilo likitokea wanahabari wenzake walikuwa wamezuiwa nje ya geti na hivyo kujikuta akiwa peke yake.

“Baada ya hapo tulichukuliwa wote mimi na walionipiga mpaka Kituo cha Polisi Usa River. Tukiwa kituoni wenzangu walimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo na kumuelezea.

“Baada ya Mkuu wa Kituo kupokea maelezo ya RPC hakuwa na sababu ya kuendelea kutushikilia na kamera yangu badala yake alituachia. Mchungaji aliyenishambulia aliniomba msamaha, tukarudi kanisani kuendelea na Ibada ya ndoa,” alisema.

Kwa upande wake, Mch. Majora akimuomba msamaha Theodora akidai kuwa zilikuwa ni hasira na hivyo alijikuta akipitiwa na kumkamata kwa nguvu kichwaji kisha kumzaba vibao.

“Naomba unisamehe, zilikuwa ni hasira tu, sisi sote ni Wakristo,” alidai Mch. Majora, wakati alipokuwa akimuomba mwandishi huyop wa habari msamaha.

Taarifa za awali kuhusu mgogoro huo wa ndoa zilidai kanisani hapo kuwa, kulikuwapo na kesi ya talaka mahakamani iliyofunguliwa na Bwana Harusi dhidi ya mke wa zamani, Aneth.

Kesi hiyo inadaiwa kuendelea bila Aneth kwenda mahakamani kutoa ushahidi wake na hivyo kuilazimu mahakama kusikiliza upande mmoja na kisha kutoa uamuzi uliobatilisha ndoa yao.

Kutokana na kushinda kesi, Bwana Harusi aliamua kufunga ndoa na mwanamke mwingine kwa kufuata taratibu za imani yake, ambapo ndoa hiyo ilitangazwa kanisani hapo.

Baada ya purukushani zilizosababisha hali ya hewa kuchafuka, ikiwamo kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa wanawake waliosababisha vurugu kanisani hapo, ndoa hiyo ilifungwa kwa amani kutokana na kutokuwapo kikwazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles