Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saady Khimji, ameipongeza Kampuni ya Ama’z Auction Mart kwa kubuni mbinu ya kuandaa mashindano ya mpira kwani yanajenga afya za wafanyakazi.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo yaliyofanyika Uwanja wa Jakaya Kikwete, Khimji ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema magonjwa mengi hasa yasiyoambukiza ni matokeo ya mtindo mbaya wa maisha.
“Siku hizi kuna matatizo ya presha, kisukari na magonjwa mengine lakini wataalam wa afya wanatuambia sababu kubwa ni mtindo mbaya wa maisha, hivyo niwapongeze Ama’z kwa hiki mlichokifanya siyo tu kwa sababu mna furaha ya kutimiza mwaka mmoja lakini mnajali afya za wafanyakazi wenu,” amesema Khimji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Ama’z Auction Mart, Dawa Jumanne, amesema waliandaa mashindano hayo kuadhimisha mwaka mmoja tangu walipozindua kampuni hiyo mwaka jana.
“Mikakati ya Ama’z ni kuendelea kuboresha huduma za udalali na huduma nyingine kupitia kampuni yetu ya usafi ili tufikie malengo tuliyojiwekea ya kutoa huduma bora kwa jamii,” amesema Dawa.
Mratibu wa mashindano hayo Rashidi Msangi, amesema yalihusisha timu za kampuni hiyo ambapo vijana wa Camp waliibuka washindi kwa mabao 6 – 0 dhidi ya wenzao wa Noah na kuzawadiwa mbuzi.