Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
BEKI wa kulia wa Yanga, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, ameruhusiwa kuitumikia timu yake hiyo, huku akitakiwa kuilipa Simba Sh milioni 120.
Kessy anatakiwa kulipa fedha hizo kwa Simba, ikiwa ni faini ya kuvunja mkataba na timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamati ya Hadhi za Wachezaji kupitia kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Alfred Lucas, zinasema kamati hiyo imekutana kupitia mapingamizi ya wachezaji na kukuta usajili wake hauna tatizo.
“Pamoja na masuala mengine, walijadili kuhusu suala la Kessy, usajili wake Yanga hauna tatizo, hivyo anaweza kuitumikia kwenye ligi, lakini anahitajika kuwalipa Simba kwa kuwa kisheria alivunja mkataba wake.
“Usajili wake si tatizo, ila kitendo cha kuvaa jezi na kuonekana akifanya mazoezi nao ndipo tatizo lilipojitokeza, kwani mkataba wake ulikuwa haujamalizika,” alisema.
Alisema kisheria mkataba ukiwa umebaki chini ya miezi sita unaruhusiwa kusaini timu nyingine lakini si kuvaa jezi, kufanya nayo mazoezi kabla ya kumalizika kabisa mkataba.
Kessy alijiunga na Yanga mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Simba, aliyoitumikia kwa miezi 17 kati ya 18 aliyojiunga nayo akitokea Mtibwa Sugar.
Beki huyo aliondoka Simba baada ya kusimamishwa michezo mitano ya mwishoni mwa ligi, kutokana na kucheza rafu katika mechi yao ya ligi dhidi ya Toto African, iliyotolewa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambao ulimalizika kwa kupokea kipigo cha bao 1-0.