NA KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kukusanya Sh bilioni 16.941, baada ya kushinda kesi tisa kati ya 10 zilizokuwa zikiwakabili wateja wao ambao walifikishwa katika Baraza la rufani za kodi Oktoba mwaka huu.
Mbali na fedha hizo, TRA imefanikiwa kukusanya Sh trilioni 1.150 Oktoba mwaka huu na kufanya makusanyo hayo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 kufikia Sh trilioni 4.752, huku lengo likiwa ni kukusanya Sh trilioni 15.1 kwa mwaka huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema makusanyo hayo yametokana na umakini wa maofisa wa mamlaka hiyo katika makusanyo pamoja na ukadiriaji halali wa kodi.
Alisema kuna jumla ya kesi 27 zinazohusu masuala mbalimbali ya kodi zilizowasilishwa katika Baraza la rufani na kati ya hizo 10 zilisikilizwa ambapo walishindwa moja na kushinda tisa, huku nyingine zikiwa bado zinaendelea.
“Ushindi huu wa kesi unadhihirisha jinsi TRA inavyofanya makadirio kwa umakini, haki na weledi bila ya kumuonea mtu yeyote na kwa upande wa makusanyo pia tunaendelea kufanya vizuri kwa sababu ya mikakati mizuri tuliyojiwekea,” alisema Kayombo.