Elizabeth Joachim
Kesi ya viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wanaokabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo uchochezi, itaanza kusikilizwa Novemba Mosi mwaka huu kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Oktoba 25, na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, baada ya Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa kupata wakili wa kumtetea mahakamani hapo, kutokana na wakili aliyekuwa akimtetea, Jeremiah Mtobesya, kujitoa Agosti 23, mwaka huu.
Wakili wake huyo Jamhuri Jonson amejitambulisha mbele ya Hakimu Mashauri na kudai kulingana na umuhimu wa kesi hiyo anaomba ahirisho ili apate nafasi ya kupitia jalada la kesi hiyo aweze kujua nini kimekwisha tokea.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi amedai mahakamani hapo, amesikia ombi la wakili wa utetezi la kuomba ahirisho ili apate muda wa kupitia jalada la kesi hiyo, hata hivyo upande wa jamhuri ulipinga ombi hilo.
Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja za upande zote mbili, ameihirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi, mwaka huu kwa ajili ya kutoa nafasi ya wakili huyo kupitia jalada na kwamba washtakiwa hao watasomewa maelezo hayo ya awali siku hiyo.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu.