26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wafundishe watoto namna ya kujali wengine  

Na CHRISTIAN BWAYA

WAZAZI bila kujali hali zenu za kimaisha, mnaunganishwa na kitu kimoja kikubwa. Sote tunatamani kuona watoto wetu wakiwa na upendo. Tunatamani watoto wetu wasiwe wachoyo, wajali hisia za watu na waishi vizuri na watu. Kujali watu ndio ubinadamu ambao usipokuwa nao huwezi kupendwa na watu wengi.

Lakini je, unapaswa kufanya nini ili kukuza watoto wenye uwezo huo? Unawasaidiaje watoto wako kuwa binadamu wenye upendo na watu? Tafiti zinaonesha mambo yafuatayo yanaweza kusaidia.

Onesha mfano

Kuwa muungwana kwa watu. Watendee watu matendo yenye utu. Heshimu watu unaoishi nao bila kujali nafasi wala hadhi zao katika jamii. Hata katika mazingira ambayo unatofautiana na watu, onesha vile unaweza kuwa muungwana kwa kutofautiana nao kistaarabu. Pale unapokutana na mtu anayefanya mambo ya kiungwana kwa wengine, ongelea jambo hilo kwa mwanao. Eleza kwanini unaguswa na kile alichokifanya. Kwa nafasi yako kama mwalimu wa kwanza wa mwanao, kile unachokisema kina nguvu ya kumgeuza mwanao.

Kwa hiyo, jiulize unaongeaje na majirani wasio na kitu kama wewe? Unaongeaje na mlinzi wa geti lako? Unaishi vipi na shemeji na mawifi zako? Watoto hawasemi lakini wako makini kusoma kile unachokifanya na uwezekano ni mkubwa hawatafanya tofauti na kile unachokifanya wewe.

 

Wafundishe ukarimu

Toa, saidia, jitolee kufanya matendo ya hisani kwa watu kuwafundisha watoto kuwa maisha ni zaidi ya kujitafutia mahitaji yenu binafsi. Matendo haya yanawafundisha kuwa thamani ya maisha inaongezeka tunapofanyika majibu ya watu wengine.

Unazo nguo mwaka umepita hujazivaa. Kuna viatu hata hukumbuki ni lini umevivaa. Kwa nini usiwape wenye uhitaji? Kuna mtu ukimpa hiyo fulana unayobana kabati lako hapo chumbani, hatalala akimshukuru Mungu kwa muujiza. Ukiitoa na mwanao akaona utakuwa umepanda mbegu itakayoota moyoni mwake.

Tenga muda nenda kanisani/msikitini kasaidie kufanya usafi ukiambatana na wanao. Nenda kwenye sehemu wanakotunza wenye mahitaji maalum wape kile ulichonacho.

 

Ishi upendo

Watu wengi wanazungumzia sana upendo lakini hawauishi upendo huo. Mnawaambia watoto wawe na tabia ya kuwasamehe wengine lakini ninyi wenyewe hamuonekani mkiwasamehe wale waliowakosea.

Ukitaka kumfanya mtoto ajifunze kujali wengine, anza kumjali yeye kwanza. Mwonyeshe huruma pale anapokosea. Usiwe na tabia ya kuweka visasi pindi mwanao anapokukosea, msamehe.

Kumbuka kuwa kila wakati unapofanya kitu kwa upendo, mtoto wako anajifunza kitu cha thamani. Ukimpenda, atashiba upendo na kwa maana hiyo atakuwa na upendo wa kutosha kuwapa na wengine.

Mzazi unaposita kumwonesha upendo mwanao, usitegemee atajifunza kuwapenda wengine. Pasipo uhakika kuwa unampenda, mwanao atakuwa na njaa ya upendo itakayomfanya awe na chuki na watu. Uhusiano wako na mwanao ndio unaojenga msingi wa vile atakavyohusiana na wengine.

Jipende

Ili mtoto awe na nguvu ya kuwapenda wengine, lazima ajipende. Kujipenda kunaanza na wewe. Lazima uoneshe kuwa unafurahia vile ulivyo. Hapa ninamaana ya kufanya kila linalowezekana kuonesha kuwa una furaha, jipende.

Huwezi kushughulika na mahitaji ya mwanao kama wewe mwenyewe umejaa kisirani. Huwezi kujali kama hujijali. Huwezi kuwapenda watoto kama hupendani na mzazi mwenzako. Ndio. Upendo kwa watoto unaanza na upendo kati yenu nyie wazazi.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles