23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KESI YA SUGU YAANZA, MSIGWA AKAMATWA

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) maarufu kwa jina la Sugu pamoja na Katibu wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho, Emmanuel Masonga wamerudishwa tena mahabusu baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama na Hakimu Mkazi, Mkoa wa Mbeya.

Awali, kesi hiyo ilifikishwa mahakamani Januari 16, mwaka huu na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Joseph Pande, ambaye aliiomba mahakama izuie dhamana kwa washtakiwa kutokana na sababu za kiusalama.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa Utetezi, Sabina Yongo ambaye aliiomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wake kwa kuwa wana haki hiyo kisheria.

Baada ya washtakiwa hao kurudishwa mahabusu, Januari 19 walifikishwa mahakamani hapo ambapo Hakimu Mkazi, Michael Mteite, alitupilia mbali ombi la Wakili Yongo la kutaka washtakiwa wapewe dhamana.

Akisoma maelezo ya awali juu ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa, Desemba 30, mwaka jana, katika mkutano wa hadhara, watuhumiwa walitoa lugha ya fedheha dhidi  ya Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa wakili huyo, siku ya mkutano huo, baadhi ya kauli za kejeli zinazodaiwa kutolewa na mshitakiwa Mbilinyi ni kwamba, Magufuli kama anataka kupendwa, asingemshuti Lissu, asingemfunga Lema miezi minne gerezani, asingenizuia nisiongee hili au lile na asingeteka watu.

Pia, Mbilinyi alinukuliwa akisema kuwa, umemteka Roma na Ben Saanane, mtoto wa watu hadi leo hatujui alipo.

Kuhusu mshtakiwa wa pili, wakili huyo alisema anadaiwa kusema hali ya maisha imekuwa ngumu, kila kona mambo yamekaza, watu wanatekwa mchana kweupe na watu wanauawa na kufungwa kwenye viroba mchana kweupe.

Katika shauri hilo, shahidi wa kwanza ambaye pia ni Mkuu wa Polisi, Wilaya ya Mbeya, James Chacha, aliieleleza mahakama, kuwa Desemba 29, mwaka jana aliwaruhusu Chadema wafanye mkutano wa hadhara, lakini akawataka wasitumie lugha za matusi.

Naye shahidi wa pili, Bonifasi Mwaitolola (34), mkazi wa Soweto jijini Mbeya, alidai siku ya mkutano watuhumiwa walitoa lugha za kuudhi dhidi ya Rais na kusababisha wananchi kugawanyika.

Naye shahidi wa tatu ambaye ni askari polisi, kitengo cha upelelezi, William Nyamakomage, siku ya mkutano alisikia watuhumiwa wakitoa lugha za uchochezi.

Hakimu Mfawidhi Mteite, aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea tena.

 

Msigwa akamatwa Iringa

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) , amekamatwa jana na polisi mjini Iringa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alipotafutwa na gazeti hili kuthibitisha tukio hilo, alisema. “Ni kweli Msigwa amekamatwa jioni hii (jana) na poli Iringa.

“Alienda polisi kutembelea viongozi wetu wako ndani zaidi ya wiki sasa, bado hatujui sababu haswa ya kukamatwa kwake kwa hiyo watu wetu wanaendelea kufuatilia kujua sababu ni nini,” alisema.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, (ACP) Julius Mjengi, kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa kutokana na simu yake kuita bila kupokewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles