NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
KESI inayomkabili Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadà mu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake imekwama, upande wa utetezi umeshindwa kupata maelezo kwamba upelelezi umefikia hatua gani kwa sababu wakili wa Serikali anayesimamia kesi hiyo hakuwepo.
Kesi hiyo ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Salum Ally ambapo Wakili wa Serikali, Anna Chimpaye alidai, amepewa maelekezo ya kuahirisha shauri hilo na kwamba wakili husika anayesimamia kesi hiyo hayupo.
Baada ya maelezo hayo, Wakili wa utetezi Fulgence Massawe alidai kesi hiyo ilipotajwa mara ya mwisho upande wa Jamhuri ulitakiwa kutoa maelezo ya hatua ya upelelezi.
Wakili Anna alidai hana maelezo ya upelelezi wa kesi hiyo hadi hapo wakili husika atakapokuwepo
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 13 ambapo upande wa mashtaka utatakiwa kutoa maelezo ya hatua ya upelelezi wa kesi.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mtaalam wa Masuala ya Tehama (ICT) Theodory Giyan kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo utakatishaji wa zaidi ya sh milioni 17.
Aprili 15 mwaka huu mahakama hiyo iliamuru upelelezi katika kesi hiyo ukamilike haraka.
“Tulifanya mawasiliano na wapelelezi kama mahakama ilivyoelekeza kukamilisha Upelelezi haraka. Wapelelezi wameahidi kukamilisha upelelezi sababu maeneo yanayopelelezwa ni mengi lakini watajitahidi wakamilishe,”alidai Wankyo Aprili 15.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh 17,354,535, kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa ya jinai na kujipatia jumla ya Sh 17,353,535 huku wakijua mapato hayo yametokana na mazalia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.