Na Clara Matimo, Mwanza
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza Machi 31, 2022 imeahirisha kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa 83 akiwemo Diana Bundala, maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kutokuwepo mahakamani hapo.
Mfalme Zumaridi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, shambulio la kudhuru mwili na kuzuia maofisa wa serikali kutimiza wajibu wao.
Kutokana na kutokuwepo mahakamani hapo kwa hakimu anayeendesha shauri hilo, Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekubora, mashauri hayo yamesikilizwa na Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga, aliiambia mahakama hiyo kwamba upelelezi wa kesi namba 11 na 12 inayomkabili mfalme Zumaridi na wanzake 82 umekamilika lakini kutokana na hakimu anayeendesha kesi hiyo pamoja na baadhi ya washtakiwa kutokuwepo mahakamani hapo ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya maelezo ya awali kusomwa.
Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14, mwaka huu ambapo mfalme zumaridi na wenzake saba ambao hawajapata dhamana wataendelea kusota rumande.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wakili wa washtakiwa hao Erick Mutta, amewaambia waandishi wa habari kwamba jumla ya washtakiwa nane wamedhaminiwa leo hivyo kufanya idadi ya ambao hawajadhaminiwa lakini dhamana yao iko wazi kufikia saba ukimuondoa mfalme Zumaridi ambaye kesi yake namba 10 ya usafirishaji haramu wa binadamu kutokuwa na dhamana.
Amesema mshtakiwa mwingine ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuugua, amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC) akiuguza majeraha aliyoyapata wakati wa kukamatwa na maafisa wa jeshi la polisi mkoani humo katika mtaa wa buguku jijini hapa.
“Kesi zote tatu leo ziliitwa, kesi namba 10 ya usafirishaji haramu wa binadamu ambayo inamuhusu Mfalme Zumaridi peke yake iliitwa kwa ajili ya kutajwa na kesi mbili zinazomkabili pamoja na wafuasi wake zilikuja kwa ajili ya usomaji wa hoja za awali.
“Lakini kwa bahati mbaya kesi hizo zote hazijaendelea kwa sababu mshtakiwa namba 38 wa kesi namba 12 hakuweza kufika mahakamani hapa yuko hospitali kwa ajili ya matibabu na kesi nyingine ambayo inamkabili mfalme Zumaridi pamoja na wenzake imeshindwa kuendelea kwa kuwa hakimu anayeendesha shauri hilo hayupo mahakamani hapa leo,”amefafanua Mutta.