NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
KESI ya uchochezi inayomkabili mgombea ubunge Jimbo la Kawe, Halima Mdee (Chadema) inatarajiwa kutajwa Oktoba 7.
Kesi hiyo iliyokuja jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya mshtakiwa kujitetea, haikuendelea kwa sababu mwendesha mashtaka hakuwepo.
Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wakili huyo ana udhuru hivyo aliomba kesi iahirishwe.
HÃ kimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7, kwa ajili ya kutajwa.
Februari 20, mwaka huu, upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ya uchochezi ulifunga ushahidi ukiwa na mashahidi watatu.
Awali Mdee alitakiwa kuanza kujitetea Julai 28, mwaka huu dhidi ya mashtaka ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli, lakini mahakama haijaanza kusikiliza utetezi.
Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Julai 3, 2017 makao makuu ya ofisi ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa ‘anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki’ na kwamba yangeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Mdee alifikishwa mahakamani hapo Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana.