Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
KESI ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imekwama kuanza kusikilizwa kwa sababu mshtakiwa anahitaji maelezo ya mlalamikaji.
Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola, alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana, kwamba wako tayari kuendelea na kesi na wanao mashahidi wawili.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, aliomba kabla ya kuanza kusikiliza mashahidi wapewe maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo.
Wakili Kongola alidai mlalamikaji katika kesi hiyo ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), na hakuwapa kwa sababu ndiye msiri wao na hawategemei kumuita mahakamani kutoa ushahidi.
Kongola alidai Jamhuri hailazimiki kutoa maelezo ya mlalamikaji ambaye si shahidi katika kesi.
“Maelezo ya ZCO ndiyo yaliyosababisha kuwapo kesi hii, maelezo ya mlalamikaji ni muhimu, naomba Jamhuri ilazimishwe kuwapa maelezo ya mlalamikaji,” alidai.
Hakimu Mkazi, Dk. Yohana Yongolo, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi kuhusu maelezo ya mlalamikaji.
Lissu anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Inadaiwa Juni 28, 2016, Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alitoa maneno ya uchochezi nje ya Mahakama ya Kisutu kwa kumuita Rais Magufuli ni ‘dikteta uchwara’.