MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi, imeahirisha kesi ya mauaji ya bilionea, Erasto Msuya kwa muda usiojulikana.
Kesi hiyo imeahirishwa jana baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kukataa kupokea gari la marehemu kama kielelezo katika kesi hiyo.
Upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana, akisaidiana na Baraka Nyambita, waliwasilisha hati hiyo mahakamani hapo kupinga uamuzi huo wa mahakama uliotolewa Januari 20, mwaka huu.
Hoja ya upande wa mashtaka ilitokana na uamuzi wa Jaji Salma Magimbi wa mahakama hiyo, kukataa kulipokea gari hilo kama kielelezo wakati shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka, Inspekta Samwel Maimu, alipotaka kulitoa kama kielelezo.
Katika shauri hilo, mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo kwa maelezo kuwa shahidi huyo siye aliyekuwa akitunza
kielelezo hicho na kwamba hata alipokuwa akitoa ushahidi wake hakuwa ameeleza alilitoa wapi gari hilo wakati akifika mahakamani.
Jaji Salma alikubaliana na pingamizi hilo la mawakili wa utetezi na kusema shahidi huyo sio mtu sahihi wa kulitoa kama kielelezo kwa vile hata ushahidi wake hauelezi alilitoa wapi wakati tayari alishahamishiwa Himo, mkoani Kilimanjaro.
“Kutokana na uamuzi wa mahakama yako, tunaomba shauri hilo liahirishwe mheshimiwa jaji.
“Pia tuna mpango wa kukata rufaa juu ya uamuzi wako wa kukataa kielelezo cha kitabu cha kumbukumbu ya kesi ya polisi,” alisema Kibwana.
Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi 13, Agosti 7 mwaka 2013, saa 6 mchana kando ya barabara kuu ya
Arusha – Moshi eneo la Mijohoroni, Wilaya ya Hai.