Na Shomari Binda, Musoma
Kesi za migogoro ya ardhi zimetajwa kuongoza katika Mahakama mbalimbali za Mkoa wa Mara kuanzia mahakama za Wilaya hadi Mahakama Kuu.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Jaji Mfawishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, John Kahyoza, wakati wa ufunguzi wa wiki ya sheria kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo, mkoani humo.
Amesema migogoro ya ardhi bado ni tatizo kubwa ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi kuanzia ngazi ya kata zinakoanzia kesi hizo.
Jaji Kahyoza amesema mabaraza ya kata yanapaswa kujikita katika kufanya usuruhishi kwenye mabaraza yao ili kupunguza kesi zinazofunguliwa mahakamani.
Amesema mabaraza yana nguvu na maamuzi yanayotolewa yapo kisheria pale pande zinazo kinzana zinapofikia muafaka kwenye usuruhishi.
“Katika Mahakama zetu bado kesi za migogoro ya ardhi zinaongoza kufunguliwa na kusikilizwa zikifuatiwa na kesi kwenye maeneo ya hifadhi za wanyama.
“Tunaendelea kutoa elimu kwenye mabaraza ya kata namna ya kusuruhisha migogoro ya ardhi na pale Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kila Alhamis kabla ya kuanza kesi tunatoa elimu kwa wananchi,” amesema Jaji Kahyoza.
Akifungua wiki hiyo ya sheria kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vicent Anney, amesema Mahakama ni muhimili ambao unafanya kazi kubwa katika utoaji wa haki.
Amesema katika kipindi hiki cha wiki ya sheria wananchi wanapaswa kutembelea mabanda yaliyopo uwanja wa shule ya msingi Mukendo ili kupata elimu mbalimbali kuhusiana na masuala ya kisheria.
Maadhimisho ya wiki ya Sheria kwa mwaka huu yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 100 ya mahakama kuu.