Kulwa Mzee -Dar es salaam
MAOMBI ya kutaka mwanahabari Erick Kabendera apewe dhamana ama afikishwe mahakamani, yamekwama kusikilizwa kwa sababu wajibu maombi wanahitaji muda kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani.
Maombi hayo namba 14 ya mwaka huu, yalitakiwa kuanza kusikilizwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai maombi yaliwafikia juzi na jana shauri limeingia mahakamani kwa mara ya kwanza.
Wankyo alidai ni matakwa ya kisheria kwamba pale panapokuwepo na kiapo, basi ni msingi wa kisheria kijibiwe kwa kiapo kinzani.
“Tunaomba mahakama itupatie tarehe ya kuwasilisha kiapo kinzani, baada ya taratibu hizo, usikilizwaji wa maombi haya ndio utakuwa na mantiki.
“Tunaomba kufaili kiapo kinzani siku ya Jumatano wiki ijayo, kesho nitakuwa Mahakama Kuu katika kesi ya uhujumu uchumi,” alidai Wankyo.
Akijibu, wakili wa mwombaji, Shilinde Swedy, alidai mteja wake yuko chini ya ulinzi kwa zaidi ya saa 24, hajapata uwakilishi wa aina yoyote hivyo aliomba shauri liwe Jumatatu.
Shilinde alisema mteja wake hajapatiwa msaada wa kisheria hadi sasa na mawakili wako wengi wanaweza kufika mahakamani kama Wankyo hatakuwepo Jumatatu ili haki itendeke.
Hakimu Rwizile alisema maombi yamekuja chini ya hati ya dharura na upande wa wajibu maombi walipewa hati ya wito Julai 31.
“Maombi ya kujibu kiapo Agosti 7 ni muda mrefu sana, maombi haya yamekuja chini ya hati ya dharura, yatasikilizwa Jumatatu Agosti 5 saa saba mchana, wajibu maombi watajibu wakati wowote kabla ya muda huo,” alisema.
Katika maombi hayo, mwombaji ni Kabendera na mjibu maombi ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Kituo cha Polisi Oysterbay, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ofisa wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Kwa mujibu wa kiapo kilichoapwa Julai 29 na Wakili Swedy kwa niaba ya Kabendera, ni kwamba mwombaji ni Mtanzania, anaishi Mbweni na anafanya kazi Dar es Salaam.
Kwamba mjibu maombi namba moja, DPP, ana jukumu la kuendesha kesi zote za jinai nchini kwa mujibu wa sheria, mjibu maombi namba mbili anamshikilia mwombaji bila kumpa dhamana ya polisi.
Mwombaji alikamatwa Julai 29 na watu sita waliojitambulish kwamba ni polisi, wakidai wanampeleka Kituo cha Polisi Oysterbay.
“Kwa mujibu wa Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, polisi wanapomnyima dhamana mtuhumiwa, lazima watoe sababu za msingi za kufanya hivyo.
“Mwombaji hajapata nafasi yoyote ya kuwasiliana na ndugu zake wala hakupewa haki ya kupata uwakilishi wa kisheria, wajibu maombi wameshindwa kumpa dhamana ya polisi mwombaji bila sababu yoyote ya msingi.
“Mwombaji ni mwandishi wa habari, anao wadhamini wa kuaminika wanaoweza kutimiza masharti ya dhamana,” alidai Swedy katika kiapo hicho.
Alidai kwa mujibu wa sheria polisi wanaposhindwa kumpa dhamana mwombaji, mahakama inayo mamkala ya kufanya hivyo kwa sababu mwombaji anayo haki kikatiba ya kuwa huru na kudhaminiwa.