28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti: Pombe ya gongo inaongeza uzalishaji mazao

Christina Gauluhanga Na Tunu Nassor– Dar es salaam

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kwakilosa ya mkoani Iringa, wamefanya utafiti uliogundua pombe aina ya gongo inaweza kutumiwa kuongeza uzalishaji mazao, kuyalinda na wadudu waharibifu.

Walisema katika utafiti wao ambao walitumia pombe hiyo kutengeneza vichocheo (homoni) vya kukuzia na kuzalishia mimea mbalimbali, ilionyesha matokeo bora kwa mimea kuzaa matunda haraka.

 Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam katika maonyesho ya Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Young Scientists Tanzania (YST), mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, Yohane Mathew, alisema ifike wakati jamii ikaona sababu ya kutumia pombe kama njia ya uzalishaji mazao badala ya kilevi.

Alisema katika utafiti aliofanya kwa kushirikiana na mwanafunzi mwenzake, Happens Masawe, walichanganya gongo na mchanga, baadaye  wakaweka kwenye moto kisha gesi iliyotoka waliikusanya na kuweka kwenye maji kisha kuifadhi  sehemu baridi.

“Baadaye hujichuja taratibu ambapo ukiichukua na kuweka kwenye mimea, inatoa majani mengi na matunda kwa wingi,” alisema Mathew.

Alisema utafiti huo walifanya kwenye mmea wa nyanya, ambapo katika kijaruba walichoweka kichocheo hicho, mimea yake ilitoa majani na matunda kwa wingi na hakikushambuliwa na wadudu.

Alisema kijaruba ambacho hakikuwekwa kichocheo hicho, kilichelewa kutoa matunda na pia kilishambuliwa na wadudu.

Mathew alisema kijaruba walichoweka kichocheo hicho, walivuna nyanya baada ya miezi miwili na wiki mbili na kile kingine kilivunwa baada ya miezi minne hadi mitano.

Alisema wakati sasa umefika kwa jamii kubadilika na kubuni viwanda vingi vya uzalishaji pombe kama vichocheo vya kilimo.

Wakati huohuo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mara iliyopo mkoani Mara, wamefanya utafiti na kubaini rangi nyeusi ni kivutio kwa mbu huku zenye mng’aro zikiwa haziwavuti.

Mmoja wa wanafunzi hao, Augustino Robert, akizungumza na MTANZANIA jana kwenye maonyesho hayo, alisema waliamua kufanya utafiti huo baada ya kuona ugonjwa wa malaria ndani ya jamii unaongezeka.

Alisema utafiti huo walifanya kwa miezi sita ambapo waliamua kuangalia rangi zinazopendwa na zisizopendwa na mbu.

Robert ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita, alisema walifanya utafiti kwa kutumia rangi nne ambazo ni udhurungi, bluu, nyeupe na njano.

“Katika utafiti huo, tulijaribu kutumia nguo za rangi hizo ambapo kila asubuhi tulikuwa tunaingia katika chumba kuangalia nguo zisizopendwa, tulibaini udhurungi na bluu ndizo zilikuwa zinapendwa sana na mbu,” alisema Robert.

Alisema katika utafiti huo, ndani ya siku saba  rangi ya udhurungi ilipandwa na mbu 103, bluu 86, nyeupe 24 na njano saba.

Aliongeza kuwa ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO)  mwaka jana, ulibaini watu 403,000  hufariki dunia kila mwaka Afrika kwa malaria.

“Hali hiyo ilisababisha pia tufanye utafiti shuleni kwetu kwa kidato cha tano ambapo tulibaini kati ya kipindi cha Januari hadi Aprili, wanafunzi 130 kati yao 35 waliumwa malaria sawa  na asilimia 27,” alisema Robert.

Alisema hivyo ni vyema jamii inapopaka rangi za maeneo mbalimbali, kuhakikisha wanatumia rangi ambazo hazina madhara, kukata majani na kufukia madimbwi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles