Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameunda mahakama maalumu kuchunguza mienendo ya Jaji wa mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, Jaji Jackton Ojwang.
Katika taarifa yake maalumu iliyotolewa katika Gazette maalumu, Uhuru alisema kuwa kuondolewa mamlakani kwa jaji huyo kutategemea matokeo ya uchunguzi wa mahakama.
Jopo la mahakama hiyo linaongozwa na Mwenyekiti wake Justice Alnashir Visram na wajumbe ni majaji Festus Azangalala, Ambrose Weda, Andrew Bahati Mwamuye, Lucy Kambuni, Sylvia Wanjiku Muchiri na Amina Abdalla.
Uhuru amesema mienendo ya Jaji Ojwang inapaswa kuchunguzwa kutokana na maswali mengi yanayoulizwa juu ya mienendo yake.
Rais Kenyatta ameongeza kuwa hatua ya kuundwa kwa mahakama maalumu dhidi ya Ojwang, imetokana na ombi lililotolewa na Tume ya huduma za mahakama ya Kenya lililowasilishwa kwake na Nelson Oduor Onyango na wajumbe wengine wanane kuhusiana na mienendo ya jaji huyo.