25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kaze ateta na wachezaji Yanga kwa saa tano

NA ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Cedric Kaze , amekutana na viongozi wenzake wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa timu hiyo na kuteta nao kwa saa tano, huku akiweka wazi msimamo wa kutowavumilia wachezaji watovu wa nidhamu na wavivu.

Kaze juzi alitembelea kambi ya timu hiyo iliyoko katika makazi maarufu ya Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam, akifanya hivyo muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuwanoa mabingwa hao mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo Mrundi ambaye amerithi mikoba ya Zlatko Krmpotic aliyeiongoza Yanga katika michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu pekee na kushinda minne na sare moja, anatarajia kuanza majukumu yake leo.

Ana kazi kubwa ya kuhakikisha Yanga inatwaa taji la Ligi Kuu, baada ya kulikosa  kwa misimu mitatu na kushuhudiwa likinyakuliwa mara zote hizo na watani wao wa jadi, timu ya Simba.

Chanzo cha habari kisichokuwa na mashaka kutoka ndani ya Yanga kililiambia MTANZANIA jana kuwa, baada ya kusaini kandarasi, Kaze aligoma kukaa hotelini na kutaka apelekwe kambini kutokana na kile alichodai kutaka kuzungumza na benchi la ufundi pamoja na wachezaji atakaofanya nao kazi.

“Kaze ni mtata sana,uongozi ulimtaka apumzike ili aende kambini leo (Jana) lakini alikataa kwa madai kwamba hana  muda wa kupoteza na muhimu akutane na wachezaji wake pamoja  na viongozi wenzake wa benchi la Ufundi, pia alitaka kuangalia miundombinu atakayotumia ili ajue anaanzia wapi programu zake.

” Alipofika kambini alikabidiwa gari na kuonyeshwa mahali atakaopokuwa akipumzika baada ya majukumu na ndipo alipotumia muda wa saa moja na nusu kuteta na Mwambusi huku akionekana kuandika vitu katika karatasi lakini pia aliwaita Meneja ( Hafidhi Salehe), Said Maulid pamoja na viongozi wengine wa benchi la ufundi kabla ya kukutana na wachezaji ambapo alitumia saa tatu na dakika kadhaa kuzungumza nao,”alisema mtoa habari huyo.

Aliendelea kufunguka kuwa, katika mazungumzo na wachezaji, kwanza aliwataka wajue wapo katika ligi kuwa hivyo wanahitaji ushindi kila mechi.

“Aliwaambia wachezaji wasijione wanacheza ligi ya Tanzania bali wachukulie ni mashindano makubwa Afrika na wanahitaji ushindi lakini alisisitiza ili wawanikiwe lazima nidhamu ndani na nje ya uwanja ipewe kipaumbele.

“Aliwaambia wazi wachezaji kwamba wakati wa kutekeleza majukumu yake nidhamu na kujituma anavipa vipaumbele na hatokuwa tayari kufanya kazi na mtu atakayekwenda kinyuma na maagizo yake,”alisema mtoa habari huyo.

Hafidhi alikiri bosi wake huyo mpya kufika katika kambi yao juzi jioni na kufanya kikao na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

“Kweli kocha alikuja jana (juzi)kambini na kufanya kikao kifupi na benchi la ufundi kisha akaonana na wachezaji na tukapata chakula cha pamoja usiku, kuhusu jambo gani alizungumza ni masuala ya ndani siwezi kuweka wazi,” alisema Hafidhi.

Katika hatua nyingine, Mshauri Mkuu wa mchakato mabadiliko ya kiuendeshaji wa Klabu ya Yanga, Senzo Mbatha ni kama amefichua siri ya mafanikio watani wao Simba, baada ya kudai kuwa timu zote alizowahi kufanya kazi zimepata mafanikio kutokana na kuwa na umoja na mshikamano ambao hata Jangwani wanahitaji kuwa nao ili kutimiza wanayohitaji.

Katika mahijiano na MTANZANIA, Senzo alisema: “Jambo la kufurahi kumpata kocha tuliyekuwa tunatamani kuwa nae, haikuwa kazi rahisi Kaze kukubali kufanya kazi na sisi. Kwa sababu hili limeshaisha jambo kumbwa lililopo mbele yetu ni kumpa ushirikiano kutoka pande zote za Yanga ili tuweze kufikia malengo yetu.

 “Kama  uongozi tumejipanga kumpa sapoti kubwa kuanzia kwenye kamati zote na menejimenti,  hivyo wadau wote wakiwamo wanachama, wapenzi na mashabiki ni muhimu sana kumpa sapoti kocha Kaze ili atimize kile ambacho Yanga inatarajia kutoka kwake na hii ndio siri ya mafanikio ya timu yoyote ulimwenguni,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles