20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Dk Shein: Barabara zinafungua ukuaji wa uchumi

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema barabara zinafungua milango na kuleta manufaa katika ukuaji na maendeleo ya uchumi na kijamii.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa kilomita 35, hafla iliyofanyika huko katika viwanja vya skuli ya Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema ujenzi wa barabara unaimarisha makaazi ya wananchi kwani walio wengi huvutika kujenga karibu na maeneo ya barabara ambapo pia shughuli za maendeleo ya biashara, kilimo, uvuvi na nyenginezo nazo huimarika.

Serikali ya awamu ya saba imejitahidi kuweka mfumo wa barabara katika hali nzuri hivyo, ni wajibu wa taasisi nyengine zinazohusika na usafiri na usafirishaji pamoja na usalama wa abiria na mizigo kushirikiana pamoja kuona kuwa ajali za barabarani zinapungua.

Alitumia fursa hiyo kuziagiza mamlaka zinazohusika kuweka alama za usalama barabarani ili ziwaongoze madereva na wapita njia katika kuzitumia barabara vizuri kwa usalama wao na vyombo vinavyoendeshwa.

Alisema kuwa kujenga barabara ni gharama lakini ikiwa zitatumika vyema na kupata matunzo mazuri gharama hizo zinafidiwa na ukuaji wa wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa jumla.

“Tumeweza, hatimae tumejenga sisi wenyewe  na mkopo wa Benki ya Kimataifa ya Nchi zinazotoa Mafuta kwa wingi (OFID) haukutosha tukaongezea wenyewe hivyo, wajue kama na sisi wenyewe tuna uwezo mkubwa”, alisema Dk. Shein.

 Rais Shein alisema barabara hiyo ni barabara ya watu wote wa Unguja na Pemba huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya UUB kwa kutengeneza barabara hiyo pamoja na kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo. 

Rais Dk. Shein alisema kwamba njia nyengine  ya kuzitunza barabara ni kujiepusha na ajali za barabarani ambapo takwimu kutoka Idara ya Usalama Barabarani zinaeleza kwamba  ajali nyingi zimekuwa zikitokea hivyo, kuna kila sababu ya kuziepuka.

Aidha, alisema kuwa kwa upande wa barabara  hiyo iliyofunguliwa leo yenye urefu wa kilomita 35 ndio ndefu zaidi kuliko barabara zote hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuitunza barabara hiyo iliyotoka Ole hadi Kengeja hasa ikizingatiwa kwamba hilo si jukumu la Serikali peke yake kwani Serikali ni watu.  

Akieleza historia fupi ya barabara kisiwani Pemba , Rais Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo inatokana na lengo na mawazo yaliyowekwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume katika kuhakikisha mtandao wa barabara unaimarika kati ya Kusini hadi Kaskazini mwa visiwa vya Unguja na Pemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles