Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo amesisitiza uchaguzi wa madiwani katika Kata ya Saranga uko pale pale licha ya vifaa vya uchaguzi kuteketea kwa moto katika Ofisi ya Mtendaji wa kata hiyo usiku wa kuamkia leo.
Kayombo amesema tayari wameshatoa taarifa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo wameahidi kuleta vifaa hivyo kati ya leo na kesho.
“Uchaguzi utafanyika tu, tumeshaangalia nini ambacho hatuna tumetoa taarifa NEC ambao wametuonyesha ushirikiano na tumekwenda nao eneo la tukio tumekagua na tumewakabidhi vile vitu ambavyo vimeteketea na wametuhakikishia tutavipata kati ya leo na kesho.
“Kwa ujumla vifaa vya uchaguzi ambavyo vilikuwapo tumekwishapanga tayari kwa ajili ya kwenda kwenye vituo vyetu 126 vingi sana vimeungua kwa hiyo tuna vifaa vichache sana,” amesema.
Aidha, Kayombo amevitaja vifaa vilivyoungua ni pamoja na masanduku ya kupigia kura 108, nyaraka za kutumika kwenye uchaguzi na za Mtendaji wa Kata na ofisi nzima vitendea kazi vya Mtendaji vyote vimeteketa ambapo hakuna kilichookolewa na kwamba thamani ya vitu hivyo haijajulikana bado hadi baada ya tathmini inayoendelea kufanyika.
Akizungumzia chanzo cha moto huo, Kayombo alisema taarifa alizopata baada ya kufika eneo la tukio ni kwamba moto ulianza saa sita na nusu usiku baada ya kuchomwa na watu wasiojulikana na wakati huo huo mlinzi wa ofisi hiyo hakuwapo.
“Watu waliokuwapo karibu waliwasiliana na mfanyakazi wa ofisi ambaye anaishi jirani na pale ambapo walifanikiwa kuokoa vitu vichache sana kama meza tatu na viti vitano na baadhi ya nyaraka,” amesema Kayombo.