MWIMBAJI wa nyimbo za injili aliyetamba na kibao cha ‘Siwema’, George Kayala, ameingia mkatabawa mwaka mmoja na Studio ya Deey Records ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya albamu yake ya pili ambayo bado hajajua ataiitaje.
Mwimbaji huyo ambaye ni mwandishi wa habari wa Burudani wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alisema amesharekodi wimbo mmoja kwenye studio hiyo iliyopo Mwembechai, jijini Dar es Salaam, chini ya prodyuza Ramadhan Lwambo.
“Huduma ya uimbaji ni sawa na huduma nyingine zinazotolewa na wachungaji, mitume, manabii, mapadri, hivyo ni
vizuri kuandaa nyimbo nzuri na kurekodiwa kwenye studio yenye ubora wa hali ya juu ili ujumbe uliokusudiwa
kuifikia jamii usikike vizuri, Deey Records ndiyo chaguo langu sahihi, ndiyo maana nimeingia nao mkataba
huo,” alisema Kayala.
Naye Deey alisema ana uzoefu wa kurekodi nyimbo za injili kwa muda mrefu, hivyo ana uhakika albamu ya Kayala itakuwa nzuri, japo wasanii wake wengi ni wa muziki wa kizazi kipya na wanaoimba mchiriku, lakini hilo halimpi
shida kukamilisha albamu ya Kayala kwa wakati waliokubaliana.