KOKU DAVID Na ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Ikulu, Peter Ilomo amesema kaya 32,461 ambazo hazina vigezo zimenufaika na mradi wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa mkutano ulioikutanisha Serikali na wahisani.
Ilomo alisema serikali imekuwa na utaratibu wa kukutana nao kila baada miezi sita kuangalia maendeleo yaliyofikiwa kwa kipindi hicho kama ni mazuri au mabaya ili yatafutiwe utatuzi.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kuna baadhi ya kaya zimenufaika wakati hazina vigezo.
Huduma imesimamishwa kwa kaya hizo huku watumishi walioshiriki kuwaingiza katika mpango huo wa kunusuru kaya masikini wamechukuliwa hatua za sheria ikiwamo kufukuzwa kazi, alisema.
“Serikali imesikitishwa kwa kitendo hicho ambacho si cha uungwana kutokana na baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu kwa kuwapa watu wasiokuwa na vigezo na hatua za sheria dhidi yao zitachukuliwa.
“Wale watu tuliowaamini wangetenda haki lakini hao hao ndiyo wamekiuka hivyo hivi sasa tunatafuta utaratibu wa namna ya kuwafikishia hizo fedha walengwa wenye vigezo ikiwa ni pamoja na kutumia kaya za eneo husika kupata kaya zenye vigezo vya kuingia kwenye mradi wa mpango wa kunusuru kaya masikini,” alisema Ilomo.
Mkurugenzi wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema zimekuwapo changamoto za watu wasio na sifa ya kuingia katika mpango huo wakati sifa zinazolengwa ni kaya zinazopata mlo mmoja kwa siku.
Alisema baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya walengwa ulifanyika uhakiki kuanzia Februari hadi Mei mwaka huu na kubaini idadi kubwa ya watu wasiokuwa na vigezo vya kuingizwa katika mpango huo.
“Kati ya kaya 32,461 tulizobaini kuwa hakuzikuwa na vigezo miongoni mwao kaya zaidi ya 8,000 zilikuwa hazina vigezo hata kimoja na tunatarajia kuzichukulia hatua stahiki.
“Wengine walioingizwa walikuwa wamekwisha kufariki dunia huku wengine walikuwa wamehama katika maeneo hayo,” alisema Mwamanga.