Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wananchi wa Kijiji cha Kauzeni kilichopo Kata ya Kibuta Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kisima kilichogharimu sh milioni 10.
Kisima hicho chenye urefu wa mita 120 kimechimbwa na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kisima hicho Kumbilamoto amesema aliguswa kukichimba ili kuwapunguzia kero ya ukosefu wa maji wananchi wa kijiji hicho ambacho yeye pia ni mwenyeji.
“Maisha waliyopitia wazee wetu ukihadithiwa unaweza ukalia, mama anaamka saa 9 alfajiri kutafuta maji, nimefanya hivi kutoa mchango wangu kwenye jamii na kumsaidia mheshimiwa rais ambaye ana kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani,” amesema Kumbilamoto.
Naye Mbunge wa Kisarawe ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, amesema jimbo hilo lina historia ya shida kubwa ya maji na kumshukuru Kumbilamoto kwa ujenzi huo.
“Kule Chole wazazi wetu walikuwa wanakwenda Mkoga au Chamayombe anaweka dumu au tofali kama foleni, anaweza akakaa siku mbili au tatu bado hajapata maji…mtu anaweza kukaa wiki nzima hajaoga na ikitokea akayapata maji basi anaoga ‘passport size’,” amesema Jafo.
Hata hivyo amesema hivi sasa maji yamefika hadi Kisarawe mjini kufuatia mradi wa kutoa maji Ruvu – Kisarawe uliogharimu Sh bilioni 10 na kwamba Serikali imetenga Sh milioni 740 na upembuzi yakinifu unaendelea kwa ajili ya kusambaza katika maeneo mengine ya jimbo hilo.
Kwa upande wake Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, ambaye alikuwa mgeni maalumu amempongeza Kumbilamoto kwa kuwa na moyo wa uzalendo na kuthamini alikotoka kwa kuwapelekea wananchi wenzake maendeleo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kauzeni, Abdallah Msanganya, ameshukuru kwa ujenzi wa kisima hicho na kusema kuwa kitawaondolea usumbufu waliokuwa wakiupata awali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo awali wananchi wa walikuwa wakipata maji kwenye visima vya asili ambavyo maji yake hayaridhishi hali iliyosababisha kusumbuliwa na magonjwa ya tumbo mara kwa mara hasa kwa watoto.