27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAULI YA RAIS MAGUFULI IWE TWISHENI KWA WANAFUNZI

Na LUCIANA LUAMBANO (TUDARCO)

WAKATI mwingine ni vema kukubaliana na maumivu ya muda ili kuponya Taifa na vizazi vijavyo.

Tujaribu kutafakari kauli ya hivi karibuni ya Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa akipiga marufuku wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kurejea na kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Akihutubia mamia ya wananchi katika Mji wa Bagamoyo, mkoani Pwani hivi karibuni, Rais Magufuli alisema ndani ya utawala wake, hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito atakayeruhusiwa kurudi shuleni.

Alisema: “Siwezi kufanya kazi ya kusomesha wazazi. Hata kama ni mtoto wangu, siwezi kumfundisha. Hilo haliwezi kutokea ndani ya utawala wangu. Sikumpeleka mtoto shule ili apate mimba.”

Kiongozi huyo wa nchi alikuwa akijibu taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), zinazotaka Serikali kuwaruhusu wanafunzi wanaopata mimba kurejea shuleni.

Juu ya hilo, alisisitiza: “Wakati mwingine ukizisikiliza hizo NGOs, utaona zinataka kulipeleka Taifa kubaya. Ndani ya utawala wangu haitatokea.

“Kama hizi NGOs zinawapenda sana hao watoto, zikafungue shule zao na kusomesha hao wazazi. Ndani ya utawala wangu, hakuna mwanafunzi yeyote mwenye mtoto atakayeruhusiwa kurudi shuleni. Serikali inatoa elimu kwa watoto, si kwa wazazi.”

Katika kupigilia msumari juu ya msimamo wake huo, Rais Magufuli aliongeza: “Hawa wanaotuletea haya mambo, hawatupendi ndugu zangu. Wametuletea dawa za kulevya, wameleta ushoga ambao hata ng’ombe hawana. Huku kuigaiga tutakuja kuiga mambo ambayo hata hayafai.”

Kwa wanafunzi ambao watapata mimba wakiwa shuleni, aliwashauri kujiunga na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) na si kurejea shuleni kuendelea na masomo.

Agizo hilo la Rais Magufuli limeonekana kupokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wadau wa elimu, lakini pia wa haki za binadamu.

Wapo waliosapoti agizo hilo, lakini wengine wakipinga wakidai kuwa linakiuka haki za binadamu, lakini pia likimnyima mtoto wa kike fursa ya kupata hitaji lake la msingi kabisa yaani elimu bora.

Katika hilo, zipo taasisi na wanaharakati mbalimbali wameanzisha mchakato wa kupingana na agizo hilo la Rais Magufuli kwa kile wanachoamini kumlinda mtoto wa kike.

Binafsi si kama ninapingana na wanaharakati hao, lakini nadhani ufike wakati agizo hilo la Rais Magufuli liwe kama darasa kwa wanafunzi wa kike.

Kama kila mmoja wetu anavyofahamu, kuna wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakijihusisha na uhusiano wa kimapenzi ambao mwisho wa siku, huwaweka katika wakati mgumu kimasomo na hata kiafya.

Sote tunafahamu kuwa mwanafunzi kujihusisha na ngono humfanya kuwa katika hatari ya kupata ujauzito, lakini pia magonjwa ya zinaa kama Ukimwi na mengineyo.

Ukiachana na hilo la magonjwa ya zinaa, lakini ujauzito umekuwa na madhara makubwa kwa ustawi wa mwanafunzi wa kike, kuanzia kimasomo na kiafya pia.

Mwanafunzi anapopata ujauzito, ni wazi atakuwa ameathirika kimasomo kwani muda mwingi atakuwa akiwaza juu ya suala hilo na kuweka pembeni masomo yake.

Lakini pia, kutokana na hali ilivyo kwa sasa katika suala zima la uzazi, ujauzito ni zaidi ya ugonjwa; tumeona wajawazito wengi wakijikuta wakipoteza maisha, huku wengine wakipata ulemavu na matatizo kadha wa kadha.

Hivyo ni vema wanafunzi wa kike kujiweka pembeni na suala zima la uhusiano wa kimapenzi ili kuepusha hatari ya kupata ujauzito wakiwa katika umri mdogo hali ambayo inaweza kuwaletea madhara makubwa.

Kila mmoja wetu anafahamu kuwa mshika mawili moja humponyoka, hivyo basi, tutumie agizo la Rais Magufuli kama twisheni kwa wanafunzi wa kike kujiweka mbali na ngono na badala yake, wasubiri wamalize masomo yao ndipo wajiingize katika mambo hayo.

Ni kwa kufanya hivyo, watoto wa kike wataweka akili zao zote katika masomo wakifahamu kuwa iwapo watajiingiza kwenye ngono na kupata ujauzito, watakuwa wameyeyusha ndoto zao walizojiwekea kama vile kuwa madaktari bingwa na nyinginezo.

Lakini pamoja na hilo, nitoe wito kwa Serikali kusaidia kuwalinda watoto wa kike dhidi ya hatari zinazoweza kuchangia kupata ujauzito bila kupenda; mathalani kupitia kubakwa na mengine kama hayo.

Sote tunafahamu jinsi shule nyingi, hasa za vijijini zilivyo mbali na makazi, hali inayowaweka watoto wa kike katika hatari ya kubakwa na mwisho wa siku, kupata ujauzito na hata magonjwa ya zinaa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ebu jamii tubadirike tatizo hili la mimba mashuleni aliwezi kutokomezwa kama tukilifumbia macho hili kupambana na haki ya mtoto wa kike ni kumjengea Elimu ya kujikinga na mausino hili kumlinda na maradhi, wana funzi tutumie kauri hii kujilinda hili na kuachana na maisha ya mausino hili tufikie malengo yetu ki Elimu

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles