NA MWANDISHI WETU, RUVUMA
KATIBU Mkuu wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, amejikuta matatizoni tena, baada ya kuachiwa kwa dhamana mkoani Ruvuma jana.
Muda mfupi baada ya kuachiwa, Dk. Mashinji aliwekwa chini ya ulinzi na kutakiwa kuripoti ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma ili ahojiwe kuhusu kauli yake ya ‘ngedere kulinda shamba’ aliyoitoa kwenye mkutano wa ndani siku chache zilizopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa mawakili wanaomtetea kiongozi huyo, Barbabas Pombona, alisema mteja wake alihojiwa kwa dakika 30.
Alisema baada ya viongozi hao kuachiliwa na mahakama kwa dhamana, Dk. Mashinji aliitikia wito wa kwenda kuhojiwa.
“Tuliwaomba polisi japo wamsubiri kwa saa moja hivi ajiandae, ndipo aende kuhojiwa, baadaye tuliitikia wito.
“RPC hatukumkuta, tulielekezwa tumwone RCO (Mkuu Upelelezi wa Mkoa). Tulimwona akamhoji kwa dakika kama 30 kuhusu kauli aliyoitoa ya kulinda shamba dhidi ya ngedere.
Alisema katika mahojiano hayo, Dk. Mashinji alihoji ngedere ni nani.
“Kwa kweli inashangaza mno, maana Katibu Mkuu amewahoji polisi ngedere ni nani, wameshindwa kumjibu,” alisema wakili Pombona.
Alisema baada ya mahojiano hayo, polisi walisema watatoa majibu Agosti 21, kama Dk. Mashinji ana kesi ya kujibu au la.
Dk. Mashinji, anadaiwa kutoa kauli hiyo alipokuwa kwenye kikao cha ndani cha Chadema wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.
Inadaiwa kuwa Dk. Mashinji akiwa katika kikao hicho, alitumia maneno ya kuudhi kwa kuwapa ushauri Watanzania kulinda mazao ya shamba lao ili yasiharibiwe na mnyama aina ya ngedere.
NJE YA MAHAKAMA
Akizungumza nje ya mahakama, Dk. Mashinji alisema kumekuwapo na presha nyingi kuhusu mikutano ya kisiasa.
“Kumekuwapo na presha kubwa ya mikutano ya kisiasa, jambo kubwa chama chetu kimekuwa makini kuhakikisha taifa letu linabaki katika hali ya utengamano.
“Kuna haki zetu za msingi ambazo zimenyakuliwa za kisiasa, tumeamua kutulia kwanza, kwa mfano sasa hivi hatuwezi tukafanya mikutano ya hadhara kama wanasiasa, tunaweza kuendelea na mikutano ya ndani ambayo taasisi zote za dola zinaelewa,” alisema.
Alisema walikamatwa na polisi kwa kosa la kukusanyika jambo ambalo halikuwa na ukweli.
“Tukiwa kwenye mkutano tulikamatwa tukaambiwa tuna kusanyiko ‘unlawful assembly’ (lisilo halali), tulivyofika polisi bahati nzuri viongozi wetu wa jimbo walikuwa wametoa taarifa ya kikao.
“Kwa mshangao tukawa ‘arrested’ na mtu yuleyule ambaye alikuwa anajua ana taarifa zetu, siye haikutupa shida tukaambiwa mtakaa saa 48 ‘remained’,” alisema.
Alisema yeye na viongozi wenzake, wamelala magereza na wamekutana na mambo makubwa.
“Tumefika magereza tumewakuta Watanzania wenzetu wengi, tumejifunza mengi, kwa watu wa nafasi kama zetu ni sehemu nzuri ambazo tunapaswa kuzitembelea mara kwa mara ili kuhakikisha tutakapopata fursa ya uongozi wa taifa hili, kuna mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyafanye.
“Tumekuwa tukifanya siasa katikia makaratasi, jana (juzi) usiku nimeona uhalisia wake, kuna vijana wengi ambao hawana ajira wanaishia katika uhalifu usio na sababu za msingi.
“Kwa nafasi zetu wanasiasa, tunatakiwa tufanye makongamano ili kuhakikisha vijana tunawatoa katika lindi la uhalifu usio na tija, hiki ni kitu ambacho nimejifunza na nitakifanyia kazi,” alisema.
Alisema mamlaka za dola zimeamua kuwasumbua, wao watii amri zao.
“Wataendelea kuwasumbua askari wetu kamata kamata ya watu, kwa sababu wao wanachukua amri, tutatii amri zao kama wao walivyotii na mahakama itaamua kama hicho kilichofanyika ni sahihi ama si sahihi,” alisema.