Na JOHANES RESPICHIUS
MWANZONI mwa wiki hii, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mikumi na nyota wa muziki wa Hip Hop nchini, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ kuhusu Serikali kuwatumia wasanii na baada ya kampeni kuwatelekeza.
Wakati akijibu alichombeza kauli iliyozua mjadala mkubwa na kuwagusa wasanii wengi, hasa wanaofanya muziki wa Hip Hop, pale aliposema hakuna msanii aliyewahi kufanikiwa kwa kuimba siasa, akiwatolea mfano Ali Kiba na Diamond Platnumz, ambao wamepata mafanikio nje ya nyimbo za siasa.
Pia aliongeza kuwa, Serikali haijawahi kumtupa msanii, bali ni wanasiasa waache kuwachochea wasanii, bali wawatie nguvu za kuwajenga, kwani muziki ni burudani na siyo siasa.
Hofu ilitanda kwa sababu maisha ya mwanadamu kwa asilimia kubwa yanaguswa na siasa, iwe afya, elimu nk, ni lazima kuna mwingiliano na siasa, hivyo kuacha kuimba nyimbo zinazohusu mambo hayo ni kuwabana wasanii, hasa wale wa hip hop, ambao wamekuwa wakiibua mambo kadha wa kadha na kuwasaidia viongozi kuyajua majukumu yao.
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ maisha yake yote ya muziki amekuwa akifanya nyimbo za siasa na amepata mafanikio kwa upande huo mpaka wananchi wamempa dhamana ya kuwawakilisha Bungeni.
Profesa Jay pia toka anaanza muziki miaka ya 90, ni msanii aliyefanya harakati zake ambazo ukizifuatilia kwa undani zimejaa mambo ya siasa mpaka akalitwaa Jimbo la Mikumi, kwa maana hiyo kuna wasanii waliofanikiwa kwa kuimba nyimbo za siasa.
Hakika kauli hiyo ilipokewa tofauti na wasanii wenyewe hata kwa baadhi ya mashabiki waliodhani kuwa Waziri amekataza wasanii kuimba siasa, ambapo kwenye kongamano la ubunifu katika kukuza uchumi Afrika Mashariki lililofanyika juzi, Dar es Salaam alitolea ufafanuzi wa kauli hiyo.
Dk Mwakyembe anasema kwamba hakukataza wasanii kuimba mambo ya siasa, ila alizungumza vile ili kufikisha ujumbe kwa wanasiasa wanaowatumia wasanii kufanikisha mambo yao kwa maslahi yao binafsi, kitu ambacho ni tofauti na dhima ya muziki ya kuburudisha.
Kwa maana hiyo, sasa wasanii waendelee kutunga nyimbo zinazohusu siasa, bila kufuata mashinikizo kutoka kwa wanasiasa ili wafanye sanaa yao vizuri, kutoa burudani, elimu na kukosoa mambo machafu kwenye jamii pale inapobidi.