26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

SERIKALI ISIPUUZE RIPOTI ZA USHAURI WA KITAALAMU SUALA LA MAJI

KAMA zilivyo nchi nyingi maskini duniani, Tanzania inakabiliwa na matatizo makubwa ya maji.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, katika nchi ambayo theluthi moja ina ukame, ni vigumu kwa watu wake kupata huduma ya maji safi na salama.

Mapema wiki hii, wakati Wizara ya Maji na Umwagiliaji ikiwasilisha bajeti yake bungeni, umeibuka mjadala mkubwa, baadhi ya wabunge wakiionya Serikali na hata kutishia kuchukua hatua endapo miradi ya maji haitafikishwa katika maeneo yao.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, yeye ameapa kuwashawishi wapiga kura wake zaidi ya 10,000 kwenda kuzima mtambo wa maji wa mradi wa Ziwa Victoria, ambao umepita katika jimbo lake ambalo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Si yeye tu, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amekaririwa akisema endapo Serikali itapuuza suala la maji, basi chama tawala kitapata wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Ripoti mpya kabisa ya Shirika la Water Aid, inaeleza kuwa, ni asilimia 56 tu ya Watanzania milioni 52 ndio wanaopata maji ya kunywa kutoka katika vyanzo ambavyo angalau vimeimarishwa.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa, asilimia 16 tu ya Watanzania wote ndio wanaopata maji safi.

Katika hali kama hii, watu maskini, hususan wanawake na watoto wa kike, wanatumia muda mwingi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Water Aid, watu milioni 14 hawana jinsi, isipokuwa kunywa maji machafu kutoka katika vyanzo ambavyo si salama.

Pamoja na hilo, Watanzania milioni 23 hawapati maji safi, huku wanawake na watoto wakitumia zaidi ya saa mbili kutafuta maji na kwa upande wa vijijini hadi saa saba.

Kutokana na hayo, ripoti hizo zimekwenda mbali na kueleza kuwa, zaidi ya watoto 4,000 wanakufa kila siku kwa magonjwa ya kuhara kwa sababu tu ya maji yasiyo salama.

Kwa ripoti hiyo na mazingira halisi ambayo baadhi yetu tumeyashuhudia ama majumbani au vijijini kwetu, utakubaliana nasi kwamba, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini ni kero kubwa.

Sababu ni nyingi, wakati mwingine ni uwezo mdogo wa Serikali katika kugharamia miradi ya maji na hivyo kusababisha usambazaji hafifu.

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit (GIZ), inaeleza kuwa, nchini Tanzania ni asilimia 23 tu ya watu wenye kipato cha chini ambao wanapata huduma ya maji ya kunywa kutoka katika shirika la umma lililopewa mamlaka ya kutoa huduma hiyo.

Pamoja na hilo, sababu nyingine zinazotajwa kukwamisha upatikanaji wa maji safi na salama ni uharibifu wa vyanzo vya maji na ongezeko la watu mijini na hivyo kuweka pengo la upatikanaji wa huduma hiyo.

Pamoja na jitihada za Serikali za kukabiliana na changamoto hizo, tunadhani ipo haja ya kuzingatia ushauri unaotolewa katika ripoti mbalimbali za kitaifa na kimataifa kuhusu kukabiliana na tatizo hilo.

Katika ripoti hizo, njia kubwa ambayo imekuwa ikishauriwa sana ni pamoja na Serikali kuhakikisha inawaweka watu maskini katika ramani yao ya kuwapatia huduma hiyo, ikiwa ni pamoja na kuweka kiwango cha bili ambacho kinaakisi gharama halisi.

Pamoja na kwamba hili Serikali imelifanya kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) la bei kutopangwa bila kushirikisha wadau, lakini bado tunadhani katika maamuzi mengi hakuna uhalisia.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles