25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

KWA HILI MISS TANZANIA MMEMUONEA DIANA

SALAMU hizi ziwafikie Hashim Lundenga ‘Anko’ na wenzake walio kwenye Kamati ya Miss Tanzania. Lundenga ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency ya jijini Dar es Salaam ambao ndiyo waandaaji wa shindano hilo.

Namwambia Lundenga na wenzake kwamba, Miss Tanzania ni shindano kubwa, lenye thamani na linalopendwa na Watanzania.

Huko nyuma kumekuwa na malalamiko mengi na wadau wameshauri mara nyingi kuhusiana na namna shindano hilo linavyoendeshwa.

Kila kukicha vinaibuka vituko baada ya vituko. Badala ya shindano kupanda thamani, linashuka.

Baada ya ushindi wa Sitti Mtemvu mwaka 2014 kulitokea sintofahamu kubwa na kuibua utata kiasi cha Sitti kuamua kuvua taji hilo na kukabidhiwa aliyekuwa mshindi wa pili, Lilian Kamazima.

Yote hayo yalipita, ikaja kashikashi ya kufungiwa na Basata na baadaye ikatoka kifungoni. Wenye kalamu zetu tukaandika, tukashauri mambo mazuri kwa Miss Tanzania yetu.

Wengi tulikuwa na imani na Miss Tanzania mpya, kwamba baada ya sekeseke basi wangeanza upya wakiwa na mabadiliko makubwa.

Wenye mapenzi mema na Miss Tanzania, tukajitia kwenye  ndege hadi jijini Mwanza, Oktoba mwaka jana ili kushuhudia fainali ya kwanza ya Miss Tanzania kufanyika nje ya Dar es Salaam.

Nilikuwepo katika Ukumbi wa Rocky City Mall, Ghana jijini Mwanza na nilishuhudia shindano hilo mwanzo mwisho. Niliripoti onyesho lile katika magazeti ya kampuni yetu. Mrembo Diana  Edward Lukumai kutoka Kinondoni  ndiye aliyeshinda.

Ni shindano lililorejea na mabadiliko makubwa, likizingatia maadili, ubora na kutokuwepo kwa upendeleo kabisa. Nilitoa pongezi zangu magazetini.

Nikiwa ukumbini pale, mwisho kabisa wa shindano lile, nilishuhudia Diana alikabidhiwa funguo za gari aina ya Toyota IST na mgeni rasmi usiku ule, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Anastazia James Wambura.

Waandishi tukawa bize kupiga picha. Duh! Kumbe ni longolongo! Ilikuwa zubaisha watu tu. Kweli mnaweza kumuingiza mkenge hata kiongozi wa serikali? Mnadanganya ni zawadi kumbe siyo?

Leo hii mnakuja kutoa zawadi baada ya miezi sita kupita, tena gari tofauti na mlilotangaza awali! IST lenyewe watu walihoji udogo wa thamani ya gari hilo, lakini leo hii imekuwa tofauti zaidi.

Hata Diana mwenyewe alipohojiwa na wanahabari juu ya maoni yake kuhusu zawadi anayopaswa kupewa mshindi wa Miss Tanzania alitaja pamoja na gari, mikataba ya uhakika ya kazi na fedha angalau Tsh milioni 50. Mnaweza kujifunza kupitia kauli yake hiyo.

Mlichofanya kwa Diana siyo haki hata kidogo. Mnapaswa mjue kuwa Miss Tanzania siyo mali yenu, ni ya Watanzania.

Ni mali yenu kama wamiliki tu, lakini wadau wanaipenda na wanajisikia uchungu inapotokea ubabaishaji wa ajabu kama huu.

Fainali Oktoba mwaka jana, zawadi Mei mwaka huu? Huu ni usanii na uswahili uliopitiliza.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles