27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

KATA MSIGANI KUNUFAIKA NA UPIMAJI ARDHI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM



ARDHI ni rasilimali muhimu mno katika maisha ya mwanadamu hapa duniani, kwani hakuna kitu chochote anachoweza kufanya pasipo kuihusisha ardhi.

Maendeleo yoyote ya mwanadamu hayaanzii juu, bali huanzia katika ardhi, anajenga na kuishi, analima na kupata chakula na mambo mengine mengi.

Wahenga walipata kusema ardhi ni mali, lakini wakati binadamu wakiendelea kuzaliana na kuongezeka, ardhi yenyewe ukubwa wake hauongezeki na hivyo yenyewe kujiongeza thamani. Katika masuala ya rasilimali ni ya pekee ambayo haipungui thamani.

Kwa msingi huo, ili ardhi iweze kumpatia manufaa mengi mwanadamu, ni lazima aipime na kuipangilia vizuri.
Leo hii tunashuhudia migogoro mingi ikiibuka katika maeneo mbalimbali nchini, baina ya wananchi na serikali yao, wananchi na wawekezaji, wakulima na wafugaji na mengineyo.

Mtaalamu wa Mipango Miji wa Kampuni ya Upimaji Ardhi ya Hosea, Renny Chiwa (Husea), anasema hali hiyo inatokea, kwani makazi mengi leo hii yamejengwa kiholela.

“Tuna ardhi kubwa na nzuri, lakini ina viraka vingi, maeneo mengi wananchi wamejenga makazi holela kiasi cha asilimia 80 ambapo ardhi hiyo haijapimwa na wala kuijapangwa,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo asilimia 80 ya Watanzania wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa ya kupoteza maeneo yao hasa serikali inapokuwa inataka kufanya miradi mikubwa ya maendeleo.

Chiwa anasema kitendo hicho cha wananchi kutopimiwa maeneo yao kinawakosesha haki na fursa nyingi, ikiwamo ya kumilikishwa kihalali maeneo yao.

“Kwa hiyo, Husea tumekusudia kuisaidia serikali kupanga miji kwa kuanzia katika ngazi ya chini kabisa ya mtaa, baadaye tutakwenda juu,” anasema.

Anasema ili kufikia lengo hilo, wanaishirikisha jamii moja kwa moja kwa kuipatia elimu kwanza kabla ya kufanya upimaji na upangaji wa ramani.

“Tunashirikiana pia na viongozi wa manispaa na mitaa husika. Kwa kuwapa elimu ya kutosha wenyeviti wa serikali za mitaa kuelewa kusudi hasa la mradi huu,” anasema.

Chiwa anaongeza: “Lengo letu ni kuiondoa kabisa hofu waliyonayo wananchi kwa kuhakikisha tunawapimia maeneo yao na kuyapanga.

“Tunataka kuiondoa kabisa ile hofu waliyonayo wananchi kwamba ipo siku watapoteza maeneo yao iwapo serikali itakusudia kutekeleza miradi mikubwa katika maeneo yao,” anasema.

Anasema kampuni hiyo imeanza muda mrefu kufanya upimaji na upangaji na kwamba inashirikiana kwa ukaribu pia na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Upimaji huu ni endelevu, katika Kata ya Goba tumepima Mtaa wa Kunguru na Mtaa wa Goba, katika Kata ya Mbezi tumepima Mtaa wa Mshikamano,” anasema.

Anasema katika Kata ya Msigani wanakusudia kupima mitaa minne ambayo ni Msigani, Temboni, Msingwa na Maramba Mawili.

“Tutahakikisha sisi wataalamu tunafanya kazi hii kwa weledi mkubwa na tunakusudia hadi tutakapomaliza tutakuwa tumewafikia na kuwasaidia takriban wananchi 32,000,” anasema.

Anasema ili kufikia lengo hilo kwa wakati, wanatumia teknolojia ya kisasa kupiga picha za juu kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani (drones).

“Wataalamu wetu wanazirusha ndege hizo juu na kupiga picha za anga ambazo zinatupa picha halisi ya makazi na jinsi maeneo husika yalivyoendelezwa kiholela.

“Kimsingi hatuwezi kuwalaumu wananchi kwa kujenga kiholela, lakini jukumu letu kuwaelimisha, kuwapimia na kuwapanga katika namna inayofaa,” anasema.

Anasema wanakusudia kufikia mwaka 2020 watakuwa wameweza kuisaidia serikali kupunguza kiwango hicho cha asilimia 80 cha makazi holela.

“Kufikia mwaka huo tutakuwa tumepunguza angalau 50 kwa 50, tunao wajibu wa kuipanga ardhi yetu, ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda tunahitaji kuwa na ardhi iliyopimwa na kupangwa vizuri,” anasema.

Anasema ardhi iliyopangwa vizuri itawavutia pia wawekezaji kuja kuwekeza kwa wingi nchini, tofauti na ilivyo sasa.
Mkurugenzi wa Husea, Pamela Marrow, anasema wanatarajia kufanya upimaji huo na kuukamilisha ndani ya miezi sita tangu hivi sasa.

Anasema upimaji na upangaji huo umekusudia kuwatambua wananchi na kuwapanga katika maeneo waliyopo na wala si kuwabomolea makazi yao kama wengi wanavyodhani.

“Kwa sababu tayari zipo ramani za mipango miji, lakini sasa wananchi imetokea wamejenga kiholela, sasa ipo changamoto ambayo tunakumbana nayo, ukosefu wa elimu.

“Wananchi hawaelewi nini tunachofanya pindi tunapokwenda kuzungumza nao, lakini tunawaelimisha kwamba lengo la mradi huu ni kuwapanga ili tuweze kupanga maeneo ya kutolea huduma za kijamii, kama vile masoko, shule na nyinginezo,” anasema.

Anasema upimaji huo ni salama kwa wananchi, kwani itawaondolea hofu ya kuondolewa katika maeneo yao na kwamba watakuwa na uhakika wamepangwa na wamepimiwa na hivyo kupata fidia kubwa watahitajika kuondolewa kwa sababu za maendeleo yao.

“Watapata hati miliki ambazo watazitumia kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha na kuinuka kiuchumi,” anasema.

Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa John Lupala, anasema lengo la wizara hiyo ni kuhakikisha kila mwaka wanatoa hati 400,000 za makazi.

“Kazi ya urasimishaji ardhi wizara tunaisimamia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kama Husea, tunaamini tutafikia lengo tulilonalo la kurasimisha ardhi kwa wananchi,” anasema.

Diwani wa Msigani, Israel Mushi, anasema kuanza kwa upimaji huo kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo.

“Lakini pia itasaidia serikali kupata mapato yake inayostahili, tofauti na ilivyo sasa, ambapo maeneo mengi hayajapimwa,” anasema Israel.

Mussa Hamza, mkazi wa Mtaa wa Msigani, anasema kuanza kwa mradi huo kumempa faraja kwamba sasa maeneo yao yatatambulika rasmi, kwani yatapimwa na watapata hati zao.

“Kupitia hati miliki tutakazopewa, tutaweza hata kupata mikopo benki, tutaaminika sasa na mikopo hiyo itatusaidia kujiendeleza kimtaji na hivyo kupata maisha bora baadaye,” anasema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Temboni, Athuman Dilolo, anasema wananchi wa mtaa huo wameitikia kwa kiwango cha hali ya juu kuhusu suala hilo.

“Lakini katika upimaji huu kuna hasara na faida ambayo itajitokeza, tunajua wazi wapo wananchi ambao wataguswa na kutakiwa pengine kuondoka katika maeneo yao.

“Ofisi ya Mtaa imepanga kuwalipa fidia wale watakaoguswa na mradi na kutakiwa kubomoa makazi yao watalipwa fidia,” anasema.

Anasema wamepanga kutenga Sh 150 katika kila mita moja ya mraba (square mita moja), fedha ambazo zitakusanywa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakaoguswa moja kwa moja na mradi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles