26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Kasusura aachiwa huru

Pg 1*Alihukumiwa miaka 35 jela, Katumikia 15

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imemwachia huru Justine Kasusura na kumfutia adhabu ya kutumikia kifungo cha  miaka 35 kwa kosa la wizi na unyang’anyi wa dola za Marekani milioni mbili (karibu Sh bilioni 4.4 kwa viwango vya sasa vya kubadili fedha)kwa kutumia silaha.

Kasusura alikaa gerezani miaka 15, ambayo tisa kati yake alitumikia kifungo na sita alikuwa rumande kwa sababu ya kukosa dhamana wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Aliachiwa huru juzi na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa; Jaji Mbarouk Mbarouk, Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles Kaijage.

 

HUKUMU JOPO LA MAJAJI

Hukumu ya jopo la majaji hao iliyotolewa Mei 9, mwaka huu, imesema Mahakama ya Rufaa haiwezi kukubaliana na upande wa Jamhuri kwamba vitendo vya mkata rufaa (Kasusura) vya kukimbia kimbia mikoani baada ya tukio la ujambazi, vingesababisha kuamini kuwa lazima alishiriki kutenda kosa hilo lililomtia hatiani.

“Kutokana na upungufu huo na mwingine, imeifanya mahakama kuamini kwamba kesi dhidi ya Kasusura haikuthibitishwa bila kuacha shaka.

“Tumeikubali sababu ya tatu ya rufaa iliyowasilishwa na mrufani kwamba ni ya msingi, hivyo tumeikubali rufaa yake, tunafuta kutiwa hatiani kwa mrufani pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka 35 jela,” lilisema jopo na kuamuru Kasusura aachiwe huru mara moja.

Hukumu hiyo inasema hati ya mashtaka ilionyesha kwamba dola milioni mbili zilizoibwa zilikuwa mali ya Citibank, lakini hakuna ushahidi ulioonyesha kuthibitisha kilichosemwa katika hati ya mashtaka.

“Ushahidi ulishindwa kuweka bayana nani alikuwa mmiliki wa fedha hizo zilizoibwa hivyo kuacha mashaka yanayompa faida mrufani.

“Tunakubaliana na mrufani kitendo cha kushindwa kumwita mahakamani ofisa kutoka Citibank ambaye ni mmiliki wa fedha hizo inaleta shaka kuamini kwamba kiasi hicho cha fedha kinachodaiwa kuibwa ndicho kilichoingia, hiyo ilisemwa awali kwamba vielelezo havisapoti kiasi cha fedha kilichokuwa katika hati ya mashtaka,” inasema hukumu hiyo.

 

KIINI CHA KESI

Kasusura na wenzake sita walishtakiwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka 2001 wakikabiliwa na mashtaka matano.

Walishtakiwa kwa kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi na mashtaka mawili ya kupokea mali inayosadikiwa kuwa ya wizi.

Kasusura aliyekuwa dereva wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support, alitumwa na meneja wa kampuni hiyo akiwa na mwenzake Said Mussa kuchukua mzigo wa fedha Uwanja wa Ndege wa Juliuis Nyerere kuupeleka Citibank.

Mussa katika ushahidi wake alidai walipotoka Uwanja wa Ndege, hatua chache walikuta gari imeegeshwa na Kasusura akaenda kuegesha gari lenye mzigo wa fedha mbele ya gari hilo.

Alidai Kasusura alimwambia kwamba mchezo umeishia hapo, akamshikia bastola akimtaka kufungua boksi lililokuwa na fedha, akachukua funguo na kulifungua, mara aliona watu asiowafahamu wakivamia na kuondoka na fedha.

Baada ya tukio hilo, Kasusura alikimbilia mikoa mbalimbali, ikidaiwa kila alipokuwa akipita alikuwa akiwapa rushwa askari na wengine walituhumiwa kumsindikiza hadi mkoani Mbeya. Hata hivyo waliposhtakiwa kwa rushwa waliachiwa huru kwakuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya polisi hao.

Kasusura alikaa mkoani Mbeya hadi Desemba 24, 2001 alipokamatwa akiwa katika nyumba ya wageni ya Moon Dust na alikana kwenda Tanga, Arusha na Sumbawanga na kueleza kwamba alipitishwa maeneo hayo na polisi.

Upande wa Jamhuri ulipofunga ushahidi wake, washtakiwa wengine waliachiwa baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu. Mwisho wa kesi iliposomwa hukumu mwaka 2007 na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Sivangilwa Mwangesi, Kasusura alitiwa hatiani baada ya mahakama kujiridhisha kwa ushahidi uliotolewa kwamba alitenda kosa.

Kasusura alihukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la wizi, miaka 30 na fimbo 12 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

 

MKEWE AFARIKI DUNIA

Siku chache baada ya hukumu hiyo, Kasusura alimpoteza mkewe ambaye alifariki dunia.

Kasusura hakuweza kupata ruhusa ya kwenda kumzika mkewe, aliyeacha motto wa kike ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kati ya tisa na 10.

Mtoto huyo alikuwa akifika mahakamani na  mama yake kila kesi ilipokuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

 

RUFAA

Baada ya kutiwa hatiani, Kasusura alikata rufaa Mahakama Kuu mwaka 2007.

Kasusura alishindwa Mahakama Kuu, lakini alikata rufaa Mahakama ya Rufaa Juni 23, 2010 akitoa sababu nane za kupinga kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa.

Miongoni mwa sababu hizo alidai Jaji wa Mahakama Kuu alijielekeza vibaya kukubaliana na hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka ulijibu kwa kwamba upande huo uliweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mrufani bila kuacha shaka yoyote.

Kweka alikubali kwamba mshtakiwa alikamatwa Desemba 24, 2001 lakini maelezo yake yalichukuliwa Desemba 26, 2001.

Alidai katika maelezo haikuonyesha kwamba kulikuwa na maombi ya kuongeza muda wa kuchukua maelezo hayo na mshtakiwa aliyakana, lakini hapakuwepo na kesi ndani ya kesi kuthibitisha maelezo hayo aliyokana yalikuwa ya kwake.

Ilidaiwa mbali na ushahidi huo wa maelezo, lakini kuna ushahidi wa mashahidi wengine uliweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

 

MAGEREZA

MTANZANIA ilipata nafasi ya kuzungumza na Ofisa Magereza wa Gereza la Ukonga (Jina tunalo, si msemaji) ambako Kasusura alikuwa alikuwa akitumiakia adhabu yake tangu alipohukumiwa kifungo mwaka 2007.

Ofisa huyo alisema Kasusura baada ya kumaliza utetezi katika Mahakama ya Rufaa, majaji waliandika hukumu na Jumatatu wiki hii iliandikwa hati ya kumwita mahakamani.

Jumanne Kasusura alipanda gari la Magereza asubuhi akiwa kavalia suti, kwenda mahakamani na ndipo alipoachiwa na kuchukuliwa na ndugu zake.

 

GEREZANI

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu maisha ya Kasusura alipokuwa gerezani, ofisa huyo alisema: “Katika kipindi chote alichokaa gerezani alikuwa mtiifu sana, mnyenyekevu, mwenye nidhamu na alikuwa mshauri mzuri wa wafungwa wengine.

“Alikuwa mnyapara (kiongozi wa wafungwa wenzake), alikuwa ni mfungwa wa mfano, alionyesha wazi kwamba alikuwa karekebishika.

“Akiwa gerezani hajawahi kufanya tukio baya la aina yoyote. Alikuwa hajui kushona, lakini alijifunza kushona akiwa gerezani na alifikia hatua ya kushona hadi nguo za wafungwa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles