25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya Escrow yamng’oa Chenge rasmi

PIX 3.

 

Na Fredy Azzah, Dar Es Salaam
WAKATI Watanzania wakisubiri hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye Rais Jakaya Kikwete alisema anamuweka kiporo kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, ametangaza rasmi kuachia nafasi hiyo.
Bunge lililopita baada ya kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, lilipitisha maazimio manane ikiwa ni pamoja na kuazimia kuwajibishwa viongozi wa Serikali na wale wa kamati za Bunge walioonekana kuhusika katika kashfa hiyo.
Viongozi wa kamati ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Victor Mwambalaswa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili lilizipata jana, Chenge alitangaza kujiuzulu nafasi yake juzi baada ya kamati yake kukutana kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
“Amejiuzulu jana (juzi), saa tano asubuhi wakati wa kikao cha Kamati ya Bajeti kilichokutana kwenye Ukumbi wa Mkwawa, ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam.
“Aliwaambia wajumbe kuwa hataki malumbano na wabunge na hataki msuguano wowote, nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na Dk. Festus Limbu, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel, alipotakiwa kuthibitisha suala hilo, alisema hayuko ofisini, hivyo hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja juu ya suala hilo.
Alisema kama Chenge mwenyewe amefikia uamuzi huo, atakuwa amempunguzia kazi Spika.
Joel alisema kujiuzulu kwake kutakuwa ni kutimiza maazimio ya Bunge jambo ambalo ni lazima litekelezwe.
Akifafanua juu ya kumpata mwenyekiti mpya wa kamati hiyo, Joel alisema mara baada ya wajumbe hao kukutana kama viongozi hawapo, jambo la kwanza ni kufanya uchaguzi.
Alisema Chenge alichaguliwa na Spika kuongoza kamati hiyo kwa kuwa ilikuwa ni kamati mpya na ambayo ni nyeti sana.
“Wajumbe wake ukiangalia wengi walitoka kwenye Kamati ya Kushauri Vyanzo Vipya vya Mapato, Spika aliomba kumchagua mtu ili apate mtu makini anayejua vyanzo vya mapato,” alisema.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kama ofisi yake ina taarifa za kujiuzulu kwa Chenge, alisema yupo jimboni na hana taarifa hizo ila anachojua suala la kuwajibika kwa wenyeviti waliotajwa kwenye ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) juu ya kashfa ya Escrow ni la lazima na halihitaji mtu kuandika barua ya kujiuzulu.
“Hakuna kuandika barua ya kujiuzulu, yale ni maamuzi ya Bunge, kinachotakiwa ni kamati kukaa na kuchagua viongozi wengine,” alisema.
Ndugai akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa juma lililopita, alisema kamati ambazo viongozi wake walihusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow, zitakapokutana jukumu la kwanza litakuwa ni kuchagua viongozi wapya kwani tayari chombo hicho kilishaazimia kuwawajibisha.
Katika kashfa ya Escrow, Chenge anadaiwa kupokea Sh bilioni 1.6, kutoka kwa James Rugamalira ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na asilimia 30 kwenye Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), inayodaiwa kuuzwa kinyemela kwa Kampuni ya Pan African Power (PAP).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles