NA SALMA JUMA
BAADA ya bifu kali kati ya kipa wa Yanga,
na Kocha mpya wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo kumalizika, kipa huyo mzoefu ameeleza kuwa kutokana na ubora alionao Maximo anaweza kuifikisha mbali timu hiyo na kufanya mambo makubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Yanga ambayo ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi msimu uliopita, inatarajia kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kaseja ambaye ni kipa wa zamani wa Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, ambayo iliwahi kufundishwa na kocha huyo kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, alisema anamkubali sana kocha huyo kuwa ni wa uhakika.
Akizungumza na BINGWA jana, Kaseja alisema Maximo ana kiwango cha hali ya juu kutokana na uzoefu wake kuifundisha timu ya Taifa, hivyo nafasi waliyoipata Yanga kufundishwa na kocha huyo itawasaidia kuwafikisha mbali.
“Jambo muhimu ni wachezaji kumpa ushirikiano na kufuata maelekezo yake mazoezini, kwani hicho ni kitu pekee kitakachoisaidia timu katika michuano ya Ligi kuu Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 23 pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.
“Ninachojua ni kuwa Maximo ni kocha mzuri, kutokana na uwezo wake alipokuwa akiifundisha timu ya Taifa, utaiwezesha Yanga kupata mambo makubwa kutoka kwake iwapo tu wachezaji watafuata kile anachofundisha,” alisema.
Hii ni kauli ya kwanza ya Kaseja ambaye hakuwa na maelewano mazuri na kocha huyo alipokuwa katika timu ya Taifa, wawili hao walimaliza bifu hilo lililozua mjadala, kilichobaki sasa ni kazi tu.
Bifu hilo lilitokea baada ya Kaseja kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu, akidaiwa kumcheka kipa namba moja wakati huo, Ivo Mapunda, baada ya kufungwa bao 4-0 dhidi ya Senegal katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika katika Uwanja wa Seghnohor uliopo mjini Dakar.
Katika hatua nyingine, Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, jana aliibuka kushuhudia mazoezi ya timu hiyo katika viwanja vya Bandari, Tandika na kuleta gumzo kwa mashabiki kwani wakati anatoka uwanjani hapo na kumsabahi Maximo, alivamiwa na mamia ya mashabiki wa timu hiyo ambao waliacha kuangalia mazoezi na kumzunguka hadi alipoondoka.
Ngassa ametoka kwenye majaribio nchini Afrika Kusini, katika timu ya Free State inayonolewa na Kocha wa zamani wa Yanga Tom Saintfiet, amefuzu lakini Yanga inahitaji dau kubwa ili imwachie.
Hata hivyo katika mazoezi hayo pia, mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Godfrey Bonny, anayechezea klabu ya Saraswot ya Nepal, alikutana na kocha Maximo ambapo walifurahi pamoja na kukumbatiana.
Yanga ilianza mazoezi yake Jumatatu wiki hii, katika fukwe ya Coco na baadaye kwenye Uwanja wa Bandari Tandika, chini ya kocha huyo mpya aliyeajiriwa na klabu hiyo hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili akitokea kwao nchini Brazil.