27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KARIBU BABU SEYA 2004-2017

BAKARI KIMWANGA NA RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BAADA ya kukaa gerezani kwa takribani miaka 13 wakitumikia kifungo cha maisha, mwanamuziki Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya na mtoto wake, Johnson Nguza (Papi Kocha), hatimaye wameachiwa huru, baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa msamaha.

Saa sita baadaye baada ya Rais Magufuli kutangaza msamaha huo, Gereza la Ukonga, Dar es Salaam liliwaachia huru Babu Seya na mwanawe.

Babu Seya na mwanawe, Papii walitoka ndani ya gereza hilo saa 12:08 jioni, huku wakiwa wamebeba magitaa mgongoni.

Wakiwa wameambatana na maofisa wa Jeshi hilo wenye silaha, Babu Seya, ambaye alivalia shati la rangi ya pinki na Papii yeye la drafti lenye rangi ya zambarau na bluu, baada ya kutoka walikutana na umati mkubwa, wakiwamo ndugu zao na wanamuziki King Kiki, Bushoke na wengine waliokuwa wakiwasubiri nje ya gereza.

MTANZANIA Jumapili, ambalo lilifika gerezani hapo, lilishuhudia watu wanaokadiriwa kufikia 100 ambao walifunga sehemu ya barabara ya kuingilia katika geti la Magereza, huku wakiimba Nguza, Nguza, hali iliyowapa furaha Babu Seya na mwanawe.

Tofauti na matarajio ya wengi, baada ya kutoka, Babu Seya na Papii hawakuzungumza chochote, zaidi waliingia katika gari dogo la rangi ya fedha aina ya Caldina namba T 670 CAW  na kisha kuelekea katika Kanisa la Life Christ Ministry, lililopo Seregerea Mwisho, ambako mtoto wake aliyeachiwa huru mwaka 2010, Nguza Mbangu, ni Mchungaji wake.

Walipofika kanisani hapo waliingia ndani wakapiga picha na kisha wakaondoka, huku Nguza akiomba waachwe wakapumzike na kuahidi kuzungumza leo.

Msamaha huo ambao Rais Magufuli aliutoa jana wakati akihutubia umma katika maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru yaliyofanyika mjini Dodoma, unaowagusa wafungwa 8,157, miongoni mwao wakiwa Babu Seya na mwanaye, umeacha bumbuwazi, mshangao na kicheko.

Babu Seya na Papi, ambao Rais Magufuli aliwaingiza kwenye kundi la wafungwa 1,828 waliotakiwa kuachiwa huru jana hiyo hiyo, walikuwa wakitumikia adhabu hiyo tangu Juni 5, 2004, baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa makosa ya kuwabaka na kuwanajisi watoto wa kike 10  wenye umri chini ya miaka 10.

Gazeti hili la Mtanzania ndilo lililokuwa la kwanza kuripoti taarifa za kukamatwa kwa Babu Seya na wanawe watatu, akiwamo Nguza Mbangu na Francis ‘Chichi’, baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, Dar es Salaam.

Baada ya kukata rufaa mbili na kuambulia patupu chini ya wakili wao, Mabere Nyaucho Marando,  ile ya mwaka 2010 ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu mwaka huo huo, Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, huku ikiwaachia huru watoto wake, Mbangu na Francis Nguza.

Msamaha wao umekuja wakati tayari wamekata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR), yenye makazi yake jijini Arusha, ambayo tayari ilikwishakutana mara tatu na kubaini kuwa, hukumu ya Babu Seya na Papii ilikuwa na kasoro.

Mwanzoni mwa mwaka huu, mtoto wa Babu Seya, Mbangu, alikaririwa na gazeti moja akisema turufu ya mwisho ya hukumu ya baba na kaka yake ni mwaka huu, wakati AfCPHR itakapokuwa inatoa uamuzi wake.

Jana wakati Rais Magufuli alipotangaza kuwaachia huru Babu Seya na mwanaye, si tu Uwanja wa Jamhuri uliolipuka kwa shangwe na pengine kuwaacha baadhi katika hali ya mshangao, bali hata katika maeneo mbalimbali.

Msamaha huo pia umekumbusha barua ya wazi iliyowahi kuandikwa na Babu Seya mwanzoni mwa mwaka huu akiilenga kwa Rais Magufuli.

Barua yenyewe ilisomeka hivi:

“Nawaomba muambieni Rais Magufuli juhudi zake nazisikia, Mungu azidi kumpa  maarifa zaidi azidi kuliongoza jahazi la Watanzania.

Rais huyu nimependa hekima zake, nami namfananisha na mwandishi wa makala za kitabu cha Methali na Muhubiri Nabii Suleimani, mwambieni Rais nimeiweka akiba yangu ya tumaini la mwisho kwake, kwani Mungu ndiye Mfalme wa kwanza anayeweza kumaliza msiba wangu huu wa kuishi kwenye kuta za magereza.

Ni yeye John Joseph anayeweza kunitenganisha mimi na maisha ya gereza, sipendi ndoto yangu ya kuja kufia gerezani, naichukia kama tawala za Herode pale Galilaya, naumwa na huku hakuna makaburi mazuri ya kuzika wafu wetu.

Mwambieni anisaidie, japo nije nifie mikononi mwa mama yangu tu aliyeteseka ‘leba’ kwa kumwaga damu zake nyingi wakati akinizaa, kama ikishindikana sio mbaya.

‘You can see my dead body through my window coffin’, mtaweza kushuhudia maiti yangu yenye pamba masikioni na puani ikiwa ndani ya jeneza langu kupitia upenyo wa dirisha la jeneza hilo, nimekinai na huku nimejifunza mengi.

Siku nitakapotoka ndiyo siku nitakapolivaa joho la uchungaji na kupita mitaani nikilihubiri neno la Mungu mpaka jasho langu ligeuke damu, natumaini katika mkono wa Bwana, natumaini katika mkono wa John Joseph haleluya! Tunaonana madhabahuni thank you!

Kila la heri Banza Stone RIP, kaka Ndanda Kosovo RIP, Amina Ngaluma (Japanese) RIP, Kakaangu Amigolasi RIP, kaka MCD RIP na wanamuziki wote mlioniacha nikiendelea kuishi kwenye kuta za gereza, Kiss you, bye!”

Kabla ya waraka huo kwa Rais Magufuli, Babu Seya na mwanawe, Juni 2014 walimwomba Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete awasamehe.

Walitoa ombi hilo kupitia wimbo wakati wakitumbuiza katika maadhimisho yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga.

Papii huku akionyesha mikono kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kububujikwa na machozi aliimba; “Kosa gani tusilosamehewa, vifungo miaka 30 jela havifundishi.

“Waziri Chikawe (Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo) tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe, hata Yesu alimkana Yesu mara tatu lakini alimsamehe, kwanini sisi?”

KAULI YA RAIS MAGUFULI

Akihutubia jana mjini hapa katika kilele cha miaka 56 ya Uhuru, Rais Dk. Magufuli, alisema ameamua kutekeleza kwa vitendo Ibara ya 45 ya Katiba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huku akinukuu ibara hiyo alisema; “Bila kuathiri masharti mengine katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anaweza kutenda lolote kati ya mambo yafuatayo:

“A. Kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote na anaweza kutoa msamaha huo ama kwa masharti au bila sharti lolote kwa mujibu wa sheria.

“B. Ibara hiyo pia inasema, Rais anaweza kumuachia kabisa mtu yeyote aliyehukumiwa au kuadhibiwa kwa kote lolote ili mtu huyo asitimize adhabu hiyo wakati wa muda maalumu na C, kulingalinisha adhabu ili adhabu tahfif, waswahili wanajua tafsiri yake vizuri, kina Kikwete (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne), sisi wa Bara hapa ni kazi ngumu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania ina wafungwa 39,000 hadi kufikia juzi ambapo kati yao, 37,000 ni wanaume na 2,000 ni wanawake.

Alisema waliohukumiwa kunyongwa ni 522, ambapo kati yao, 503 ni wanaume na 19 ni wanawake.

“Waliohukumiwa kifungo cha maisha ni 666, ambapo kati yao wanaume ni 655 na 11 ni wanawake. Kwa mujibu wa ibara hii ya 45 na hasa kwa kuzingatia kuwa sisi ni binadamu.

“Nimeamua kuwasamehe wafungwa 8,157 ambapo wafungwa 1,828 watatoka leo (jana) na 6,329 wamepunguziwa muda wa kukaa gerezani na watatoka kwa mujibu wa vifungo vyao. Lakini pia kwa mujibu wa ibara hiyo hiyo ya 45, wapo waliohukumiwa kunyongwa, wapo wenye umri zaidi ya miaka 85. Pia wapo wafungwa ambao waliotubu kweli dhambi zao.

“Ndugu zangu baada ya kukaa na kufikiria na kwa sababu sisi wanadamu kila siku huwa tunaomba kusamehewa. Nimeguswa ndugu zangu Watanzania na hasa ukiangalia hawa waliofikisha mpaka miaka 85 ni wazee na hii nimepata taarifa ya magerezani,” alisema.

Rais Magufuli pia alisema ameamua kuwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa na kuwataka wahusika wafanye mchakato wa kuwatoa jana au leo.

“Yupo mzee mmoja anaitwa Mganga Matonya ana miaka 85 na amekaa gerezani miaka 37 na mahabusu miaka 7, ukimjulisha hii utaona amekaa gerezani miaka 44. Ninaomba orodha hii nitamkabidhi Waziri Mkuu awashughulikie,” alisema.

IBARA ILIYOTUMIKA KUMSAMEHE BABU SEYA NA MWANAWE

Rais Magufuli pia alitumia ibara hiyo hiyo ya 45 kutoa msamaha kwa familia ya Babu Seya.

“Kwa mujibu wa ibada hii ya 45, pia ninatoa msamaha wa kuachiwa huru familia ya Nguza Viking, jina lingine anaitwa Babu Seya na mwanawe ndugu Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ nao waachiwe huru,” alisema.

Rais Magufuli alionya na kusema kuwa msamaha huo hautawahusu wale waliofanya vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino pamoja na ujambazi.

MREMA KUMTEMBELEA BABU SEYA

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustino Mrema, mbali na kumpongeza Rais Magufuli kwa kufanya uamuzi aliouita kuwa ni wa kihistoria, alisema atakwenda kumtembelea Babu Seya nyumbani kwake.

Mrema, ambaye alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, mbali na kusema Babu Seya ni kama ndugu yake kutokana na kuishi pamoja katika eneo la Sinza, alisisitiza juu ya nguvu ya kusamehe.

“Wengine wamekwishaanza kusema Rais Magufuli amevunja sheria, huu ni unafiki, wasome Katiba inampa Rais Mamlaka ya kubadili kifungo cha kunyongwa kuwa cha maisha, Babu Seya hata kama alifanya kosa amekwishajutia, tujifunze kusamehe tusiishi kwa chuki na visasi,” alisema Mrema.

Katika hilo, Mrema alisema Rais Magufuli ameonyesha ubinadamu na anaamini kutokana na hulka yake ya udadisi amethubutu kuingia magereza na kuona shida nyingi, ikiwamo msongamano wa wafungwa.

Alisema wao kama Bodi ya Parole, moja kati ya mambo ambayo waliamua kushughulikia ipasavyo ni suala la msongamano wa wafungwa, lakini kwa bahati mbaya walikwamishwa.

“Mimi nilijaribu hilo, tulikwenda Gereza la Isanga, Dodoma tuligundua kuna wafungwa 80 ambao walishindwa kulipa faini wakafungwa, nikamtafuta Mchungaji Getrude Rwakatare akakubali kutoa milioni 12  tukahesabu wakapatikana 43 wa kuwalipia tukaenda nao mahakamani, mahakama ikakubali, lakini baadaye wakakataliwa eti nikaambiwa hawawezi kujutia makosa, labda hiyo faini ilipwe na ndugu zake, nikajiuliza hao ndugu zake ni akina nani?” alisema Mrema na kusisitiza kuwa, kule gerezani kuna mawazo potofu.

Mrema alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kuliona hilo, na kutumia Katiba na kufanya maamuzi pasipo kuogopa lawama.

Alipoulizwa anazungumziaje endapo Rais Magufuli akitumia mamlaka hayohayo kuwaachia huru masheikh wa Uamsho waliopo gerezani wanaotuhumiwa kwa ugaidi, Mrema alisema kwa kuwa suala hilo ni tatizo kubwa la kidunia, anaamini Rais Magufuli hawezi kukubali mtu awekwe ndani bila sababu za msingi na kushauri atumie vyombo vyake kuchunguza jambo hilo.

Awali akizungumza katika uwanja wa Jamhuri mkoani hapa, mara baada ya Rais Dk. Magufuli kutangaza kuipa msamaha familia ya Babu Seya, Mkurugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema alilia mara baada ya Rais Magufuli kutamka msahama dhidi ya Babu Seya na mwanawe.

“Nimelia, nimetoa machozi ya furaha, Rais amefanya jambo jema sana, kila mmoja alikuwa akimwombea Babu Seya ili aweze kutoka, hakika ameifanya nchi yetu iheshimike sana nje ya nchi,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Molel (CCM), alisema Serikali ilikuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kulisha wafungwa, hivyo kitendo cha Rais Dk. Magufuli kutoa msamaha ni kizuri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kutoa msamaha kwa wafungwa, huku akimtaka kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.

“Ni vizuri, ni vizuri sana, amefanya jambo zuri, hakika huu ni uungwana, ila bado tuna changamoto nyingi katika miaka yetu hii 56, kwani takwimu zinaonesha asilimia 33 ya watoto wana utapiamlo,” alisema.

WIZARA YAFAFANUA MSAMAHA

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilitoa taarifa na kufafanua msamaha ambao Rais Magufuli aliutangaza kwa wafungwa 8,157.

Taarifa  iliyotolewa jana kwa vyombo vya Habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira, ilieleza kuwa, kati ya hao 6,329 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huo.

Akifafanua zaidi, alisema Ibara ya 45(1) (d) ya Katiba ndiyo inampa mamlaka Rais kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote.

Katika taarifa hiyo, Rwegasira alisema kuwa, wafungwa wengine waliosamehewa ni wale wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na saratani, ambao wako kwenye hatua za mwisho ambao walipaswa kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Alisema wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi.  Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Alisema msamaha huo pia unawahusu wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

“Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili. Ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya,” alisema Meja Jenerali mstaafu Rwegasira.

Meja Jenerali mstaafu Rwegasira alisema msamaha wa Rais hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua.

Wengine ni wale waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

Aliwataja wengine kuwa ni waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bangi n.k.

Alisema pia hauwahusu wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo.

Alisema wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali na wale wa kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, ukatili kwa watoto au kujaribu kutenda makosa hayo pia haitawahusu.

Alisema msahama huo pia hauwahusu waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

Aliwataja wengine ambao hawaguswi na msahama huo kuwa ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

Wengine ni wale wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii na waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na kuhujumu uchumi.

Alisema msamaha huo pia hautawahusu wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Wafungwa wengine ambao hawataguswa ni wale waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo, hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu.

Alisema wasioguswa pia ni wale waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu, vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili.

Aliwataja wengine kuwa ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali, wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali, walioingia gerezani baada ya Oktoba 30, 2017 na waliowahi kufungwa gerezani.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Tom Nyanduga, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kuwafutia adhabu ya kifo watu 61 waliokuwa magereza mbalimbali nchini, wakisubiri utekelezaji wake.

Nyanduga alisema uamuzi huo unaendana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 62/149 la Desemba 18, 2007 linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta au kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles